Wito kutambua wanaojitolea kuhudumia jamii
HUKU ulimwengu ukikabiliwa na misukosuko inayozidi kuongezeka kuanzia janga la athari za tabianchi, migogoro, na hali ya kiuchumi isiyotabirika, ipo nguzo muhimu ambayo licha ya hayo inajizatiti kuwa mstari wa mbele kuhudumia jamii.
Wanaojitolea, kwa Kiingereza, volunteers, wanahatarisha maisha yao, na Desemba 5 kila mwaka hukumbukwa kama nguzo muhimu katika jamii.
Kwenye maadhimisho ya mwaka huu, Muungano wa Umoja wa Mataifa (UN), ulitangaza kuwa 2026 utakuwa mwaka wa Kimataifa wa Kujitolea, UN ikisema hatua hiyo ni wito wa kimataifa kwa serikali, taasisi na jamii kutambua jukumu la wanaojitolea kikazi – kama nguzo ya maendeleo na uthabiti.
Ulimwenguni, zaidi ya watu bilioni 2.1 hujitolea kila mwezi kuhudumia jamii kwa njia moja ama nyingine — hii ikiashiria takwimu ya mtu mmoja kati ya watu watatu wanaofanya kazi.
Majukumu yao yanahusisha kukabiliana na majanga, dharura, kulinda mazingira, kuongoza vijana na kusaidia jamii, mara nyingi hata kabla ya taasisi rasmi zilizotwikwa majukumu kujitokeza.
“Wanaojitolea hawaangazii gapu zilizopo pekee, bali pia wanafanikisha maendeleo na kuleta utangamano kwenye jamii,” akasema Louise Chamberlain Naibu Mkurugenzi wa Uratibu Kitengo cha Kujitolea cha UN, wakati wa maadhimisho ya 2025 jijini Nairobi.
Afisa huyo, aidha, aliongoza msururu wa mashirika ya uhisani kuadhimisha siku hiyo maalum ulimwenguni.
Hotuba zilizotolewa na wadauhusika mbalimbali, nchi za Kusini mwa Dunia zilitajwa kama zinazojitolea zaidi ila jitihada zao zinaashiria kuambulia patupu.
Barani Afrika, asilimia 58.5 ya watu hujitolea kila mwezi kuhudumia jamii — kiwango cha juu zaidi duniani.
Mifumo ya jadi ya kusaidiana kama umuganda nchini Rwanda na harambee nchini Kenya, imeendeleza jamii kwa vizazi, ikijenga uaminifu na uwajibikaji wa pamoja.
Leo hii, kazi za kujitolea barani zinaendelea kujitokeza, zikiwa ni za kisasa na zenye manufaa kiuchumi.
Kulingana na UN, Kenya ni nchi yenye mfano mzuri wa watu wanaojituma kuhudumia jamii bila malipo takwimu zikionyesha kila mwaka kundi hilo huchapa kazi kwa muda wa saa milioni 669 — sawa na asilimia 3.66 ya Pato la Taifa (GDP).
Aidha, Sheria ya Kitaifa ya Kujitolea nchini inaainisha hatua ya kujitolea kuhudumia jamii kama ya kimikakati kuboresha taifa bali si tendo la uhisani.
Rwanda, kupitia umuganda, inaendelea kujenga shule, kuboresha miundomsingi na kuimarisha umoja wa raia.
Ethiopia kwa upande wake, wanaojitolea wana mchango mkubwa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, dharura na utoaji wa huduma za kimsingi.
Nchini Sudan Kusini, vijana wanaojitolea wanasaidia majadiliano ya kijamii na kuhamasisha umoja na utangamano katika maeneo yanayoendelea kupata utulivu kufuatia migogoro.
Licha ya udhaifu wa mifumo, kujitolea bado ni nguzo muhimu katika ukuaji wa jamii na taifa. Mchango mkubwa wa wanaojitolea, hawaonekani katika mifumo ya kitaifa ya takwimu.
Ni nchi chache zinazonakili data za wanaojitolea, ikiwa ni pamoja na kutambua thamani yao. Bila takwimu, wanaojitolea mhanga hawatambuliki kwenye sera na bajeti.
Kenya, wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Mashujaa kila mwaka kiongozi wa nchi aliye madarakani huwapa taji wanaojitolea kuhudumia taifa kwa njia moja ama nyingine.
Ripoti ijayo ya Hali ya Ujitoleaji Duniani (SWVR) 2026 inalenga kubadilisha hali hii kupitia Global Index of Volunteer Engagement (GIVE), mfumo mpya unaokusudiwa kupima thamani kamili ya kazi za kujitolea huku ikiheshimu uhalisia wa maeneo mbalimbali.
GIVE ina uwezo wa kubadili jinsi nchi zinavyopanga, kugawa rasilimali na kujenga uthabiti wa kitaifa.
Lakini takwimu pekee hazitoshi. Ujitoleaji lazima uwe wa kujumuisha. Wanawake, vijana, watu wenye ulemavu na jamii za vijijini, ndio uti wa mgongo wa kundi la wanaojitolea Barani Afrika, ingawa mara nyingi hukumbana na vikwazo vikubwa zaidi.
Takwimu zilizogawanywa kwa misingi ya jinsia, umri na ulemavu ni muhimu ili kuhakikisha ushiriki wa haki.
Mwaka 2026 unapokaribia, UN, serikali, mashirika ya kutetea haki za kijamii na kibinadamu, wataalamu na sekta ya kibinafsi, wote wanahimizwa kuwekeza raslimali za kutosha kwenye ajenda za kujitolea kuhudumia jamii, kuhakikisha uwepo wa mazingira salama, na kuwa na teknolojia bunifu kuimarisha ushirikiano wa kikanda.