Ombi mshukiwa wa mauaji ya wagonjwa KNH Kalombotole apimwe akili kwa mara ya pili
MSHUKIWA mkuu katika mauaji ya wagonjwa katika Hospitali Kuu ya Kenyatta, Kennedy Kalombotole amerudishwa rumande kusubiri uamuzi iwapo atapimwa utimamu wa akili yake.
Mawakili Joshua Ombengi, Philip Maiyo na Zephania Achapa walimsihi Jaji Diana Kavedza, Mahakama Kuu ya Kibera, aamuru Kalombotole apimwe mara ya pili ibainike ikiwa anaweza kujibu kesi ya mauaji ya mgonjwa- Gilbert Kinyua Muthoni.
Kalombotole ameshtakiwa kwamba mnamo Julai 17, 2025 alimuua Gilbert Kinyua Muthoni aliyekuwa amelazwa katika hospitali kuu ya KNH Wodi nambari 7B.
Jaji Kavedza aliamuru Kalombotole azuiliwe hadi Oktoba 22, 2025 atakapoamua ikiwa ataamuru mshtakiwa afanyiwe ukaguzi tena au la.
Mahakama ilisema ripoti iliyowasilishwa na kiongozi wa mashtaka ni kwamba “Kalombotole yuko na akili timamu na anaweza kujibu mashtaka dhidi yake.”
Bw Ombengi alimweleza jaji kwamba inafaa madaktari zaidi ya mmoja kumpima Kalombotole ikiwa yuko na akili timamu.
“Naomba hii mahakama isitishe kumsomea mashtaka Kalombotole had kuwe na ripoti nyingine ya kuthibitisha utimamu wa akili yake,” Bw Ombengi alimsihi Jaji Kavedza.
Jaji huyo alimweleza mshtakiwa anayezuiliwa katika gereza la viwandani kwamba atasubiri hadi Oktoba 22,2025 uamuzi utakapotolewa ikiwa atapimwa akili tena au la.
“Umesikia vile mahakama imesema,” Jaji Kavedza alimwuliza Kalombotole ambaye kwa muda amekuwa hazungumzi.
Alikuwa akizungumziwa na mahakama kama amenyamaza kabisa kana kwamba ni bubu.
“Ndio nimesikia. Naomba mahakama iwe inazungumza Kiswahili. Sielewe kimombo,” Kalombotole alimweleza Jaji Kavedza.
Jaji huyo alifurahi kuzungumza na mshukiwa huyo anayechunguzwa na polisi kwa mauaji ya wagonjwa KNH.