Wito Ruto arekebishe sheria ya Matumizi mabaya ya Kompyuta
SHINIKIZO linaongezeka kwa Rais William Ruto kuangazia upya sheria tata ya Matumizi Mabaya ya Kompyuta na Uhalifu wa Mtandao.
Haya yanajiri baada ya Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu nchini (KNCHR) kuitaja Sheria hiyo mpya kuwa yenye kasoro za kisheria na yenye kukandamiza uhuru wa kujieleza na haki ya faragha.
Baraza la waangalizi wa serikali lilitoa wito kwa serikali na Bunge kupitia na kurekebisha sheria hiyo ambayo walisema inawaweka wanaokosoa serikali hatarini.
Wakifika mbele ya kamati ya Uwiano ya Kitaifa ya Seneti, Tume hiyo ikiongozwa na mwenyekiti wake mpya Claris Ogangah na Martin Pepela ilishikilia kuwa sheria hiyo mpya haikidhi viwango vya uhalali, uwazi na uwiano, kinyume na katiba.
Tume hiyo ilisema vifungu kadhaa vya sheria hiyo mpya vinakiuka haki kadhaa zisizoweza kupuuzwa ikiwa ni pamoja na uhuru wa mawazo na kujieleza pamoja na haki ya faragha.
‘Kwa kuharamisha matamshi ambayo yanaonekana kuwa ya kuudhi, yanayochukiza au yasiyofaa, Kenya inahatarisha utiifu wake wa majukumu ya kimataifa chini ya sheria mbalimbali za kimataifa,’ alisema Bi Ogangah.
Ikifadhiliwa na Mbunge wa Wajir Mashariki Aden Mohamed, lengo la sheria hiyo mpya lilikuwa ni kupiga marufuku matumizi ya kompyuta kuendeleza ugaidi na dini potovu.
Hata hivyo, Sheria mpya imeibua wasiwasi kutoka kwa wananchi na taasisi, ikitaja uwezekano wake wa kukiuka haki za kimsingi na uhuru unaotolewa chini ya Katiba.
Jumuiya ya Wanasheria nchini na Tume ya Haki za Kibinadamu ziliwasilisha maombi tofauti ya kutaka kutangazwa kuwa vipengee kadhaa vya Sheria hiyo vinakiuka Kifungu cha 31 cha Katiba na Kifungu cha 25 na 27 cha Sheria ya Kulinda Data.
Kwa sababu hiyo, Mahakama Kuu ilisimamisha Vifungu viwili vya Sheria iliyolalamikiwa, Kifungu cha 27(1) na (2) kusubiri kusikilizwa na uamuzi kutolewa.