Makala

Wito Sakaja alipe wanakandarasi

Na WINNIE ONYANDO September 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

GAVANA wa Nairobi, Bw Johnson Sakaja, ametakiwa kuwalipa wakandarasi waliotoa huduma kwa Kaunti ya Nairobi ili huduma muhimu zirejee katika hali ya kawaida.

Mbunge wa Embakasi Kaskazini, James Gakuya, alisema kukosa kulipwa kwa wakandarasi hao kumesababisha huduma nyingi kusimama, hasa ukusanyaji wa takataka katika mitaa mbalimbali ya jiji.

“Ni aibu kuona taka zikizagaa mitaani ilhali wakandarasi walishafanya kazi yao na hawajalipwa. Hali hii inawaathiri wakazi moja kwa moja,” Bw Gakuya alisema Jumatano Septemba 24,2025.

Kauli yake iliungwa mkono na diwani wa Wadi wa Nairobi South, Bi Waithera Chege, aliyemshutumu Bw Sakaja kwa kutelekeza majukumu yake.

Diwani wa Wadi wa Nairobi South, Bi Waithera Chege akiwahutubia wakazi Septemba 24,2025. PICHA|WINNIE ONYANDO

Alisema miradi mingi ya maendeleo imesimama katika wadi kadhaa kwa sababu ya ufadhili kukosekana.

Bi Chege aliongeza kuwa wanafunzi kutoka familia zisizojiweza pia wameshindwa kuendelea na masomo kwa kukosa karo baada ya serikali ya kaunti kushindwa kutenga fedha za msaada.

Viongozi hao wawili waliwataka wakazi wa Nairobi kuwapigia kura viongozi wenye maono na dhamira ya maendeleo katika uchaguzi mkuu ujao.

Haya yanajiri huku diwani wa wadi ya Githurai Deonysias Mwangi Waithira akitangaza kuwa atajiuzulu kufikia Novemba 1, akisema anahangaishwa na utawala wa Gavana Sakaja.

Diwani huyo anadai kuwa utawala wa Bw Sakaja hautekelezi miradi ya maendeleo kwenye wadi yake.

“Nilikuwa nimeamua kujiuzulu jinsi ambavyo imenakiliwa kwenye barua na niseme nitafanya hivyo Novemba 1, 2025. Hata hivyo, watu ambao wataamua mustakabali yangu ni watu wa Githurai,” Bw Mwangi alisema kwenye kipindi cha Fixing the Nation kinachopeperushwa na NTV Septemba 23,2024.

Hata hivyo, hii sio mara ya kwanza tetesi kama hizo kuibuliwa.

Wafanyakazi wa kaunti pia wamekuwa wakilalamika kutopokea mishahara yao.

Wiki moja iliyopita, wafanyikazi wa Kaunti ya Nairobi waliagizwa kupunguza kasi ya kazi zao au kubaki nyumbani hadi mishahara yao itakapoongezwa, kufuatia kucheleweshwa mara kwa mara na kuwafanya wafanyikazi kushindwa kutimiza majukumu ya kibinafsi na ya kifamilia.

Katika barua iliyoandikwa Septemba 17, 2025 na kutumwa kwa Gavana Sakaja, Chama cha Wafanyakazi wa Serikali ya Kaunti nchini (KCGWU) kilisema mishahara ya wafanyakazi hao ya Julai na Agosti bado haijatolewa.

“Inasikitisha sana kwamba leo, Septemba 17, wafanyikazi wa kaunti ya Nairobi bado hawajapokea pesa zao kutoka Julai na Agosti 2025, na hakuna dalili za wakati mishahara hiyo italipwa. Huu ni ukiukaji mkubwa wa makubaliano yetu,” muungano huo ulisema.