Wito serikali iboreshe usimamizi wa fedha za NG-CDF
RAIS wa Bunge la Mwananchi, Francis Awino, ametoa wito kwa serikali kuchukua hatua za haraka kuimarisha usimamizi wa fedha za Hazina ya Maendeleo ya Maeneobunge (NG-CDF) na basari.
Bw Awino anadai kuwa pesa hizo ambazo zinafaa kuwafaidi wanafunzi zinapotea mikononi mwa viongozi wachache wenye tamaa.
Akizungumza Jumamosi, Jivanjee jijini Nairobi, Bw Awino alilalamikia jinsi watoto wengi wanalazimika kukaa nyumbani kwa sababu ya ukosefu wa karo huku wazazi wakiendelea kutaabika.
“Ni kinaya kuwa pesa ambazo zinafaa kuwasaidia watoto wetu zinaingia mfukoni mwa viongozi wenye tamaa,” akasema Bw Awino.
Alisisitiza kwamba fedha hizi zinapaswa kuelekezwa moja kwa moja katika mfumo wa elimu badala ya kupitia mikononi mwa watu wenye taa wanaoonekana kuzitumia vibaya.
“Fedha hizi zilitengwa kwa ajili ya kusaidia maskini na kuelimisha watoto wetu. Lakini fedha hizo zinapotea mikononi mwa viongozi wachache walafi. Wazazi wanateseka, watoto wetu wanakaa nyumbani kwa sababu hawawezi kulipa karo. Serikali inapaswa kuelekeza fedha hizi moja kwa moja kwenye mfumo wa elimu ili kuboresha sekta ya elimu, na kufanya elimu iwe nafuu kwa mwananchi wa kawaida,” alisema Awino.
Kuhusu suala la bajeti ya kitaifa, Bw Awino aliikosoa vikali serikali kwa kupanga bajeti bila kushirikisha umma.
Ametoa wito kwa Waziri wa Fedha, John Mbadi, na Hazina ya Kitaifa kushirikiana na wananchi ili kuhakikisha bajeti hiyo inaakisi mahitaji halisi ya wananchi wa kawaida.
“Bajeti za kitaifa haifai kuundwa ofisini bila kuwahusisha wananchi. Umma unafaa kushirikishwa,” aliongeza.
Haya yanajiri huku wabunge wakijitayarisha kushirikisha umma kote nchini kuhusu Mswada wa Marekebisho ya Katiba wa mwaka 2025.
Mswada huo, uliodhaminiwa na Mbunge wa Rarieda Otiende Amollo pamoja na mwenzake wa Ainabkoi Samuel Chepkonga, unalenga kukita kwenye Katiba: Hazina ya Maendeleo ya Maeneobunge (NG-CDF), Hazina ya Usawa ya Serikali ya Kitaifa (NGAAF), na Hazina ya Usimamizi ya Seneti.
Ushirikishaji wa umma kuhusu mswada huu utafanyika kuanzia Mei 5 hadi Mei 7, 2025 katika maeneobunge yote na kaunti.
Hata hivyo, viongozi wa kisiasa kama Raila Odinga wamepinga NG-CDF, wakidai kuwa ni njia ya wabunge kuingilia majukumu ya serikali za kaunti.
Akizungumza wiki jana kwenye mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Kisumu Ken Nyagudi, Bw Odinga alitishia kuwa NG-CDF itakuwa ajenda kuu ya kampeni za 2027 endapo haitabadilishwa.
Lakini wabunge wamekaidi msimamo huo na kuendelea kushinikiza Wizara ya Fedha kuachilia fedha hizo, wakisema wanafunzi maskini wanazitegemea. Aidha, wabunge wanasema bila NG-CDF, wengi wao huenda wakapoteza viti vyao 2027.