Makala

Wito wahudumu wa bodaboda wawe makini, wajilinde wakiwa barabarani

Na WINNIE ONYANDO January 28th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

KAMPUNI ya biashara ya sarafu za kidijitali, Binance, imezindua kampeni ya kuwahamasisha wahudumu wa bodaboda kuhusu umuhimu wa kudumisha usalama wao barabarani.

Kampeni hiyo, iliyopewa jina la Safety Campaign, ilizinduliwa jijini Nairobi Januari 28, 2026 wakati wa Data Privacy Week na inalenga kuunganisha mazoea ya kila siku ya usalama na ulinzi wa fedha na taarifa binafsi mtandaoni

Katika hafla hiyo, wahudumu wa bodaboda walipewa helmeti na mavazi rasmi na hata kufunzwa kuhusu usalama barabarani.

Hatua hiyo inalenga kufafanua kwa njia rahisi umuhimu wa kujilinda, sawa na hatua zinazochukuliwa kulinda mali za kidijitali.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Kiongozi wa Operesheni wa Binance Afrika, Saruni Maina, alisema kuwa usalama iwe barabarani au mtandaoni ni muhimu sana.

“Vaa helmeti kujilinda barabarani, vivyo hivyo chukua hatua za usalama unaposhiriki katika uchumi wa kidijitali,” alisema Bw Maina.

Naye rais wa Chama cha Madereva wa Kidijitali na Usafirishaji nchini, Calvince Okumu, alisema mpango huo umekuja wakati mwafaka kwani unazingatia changamoto halisi zinazowakumba wahudumu wa bodaboda.

“Wengi wetu hatuwezi kumudu vifaa bora vya usalama. Kupokea helmeti hizi ni hatua muhimu na pia imetufungua macho kuhusu kulinda kipato chetu mtandaoni,” alisema Okumu

Kampeni hiyo itaendelea kupitia mitandao ya kijamii, ushirikiano na washawishi pamoja na maudhui ya elimu, huku ikilenga kujenga mazingira salama na jumuishi ya matumizi ya sarafu za kidijitali barani Afrika.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi Barabarani (NTSA) kuzindua mpango wa kutoa vipimo vya macho vya lazima bila malipo kwa madereva wote jijini Nairobi, kufuatia ongezeko kubwa la ajali barabarani mwaka huu.

Katika siku 20 za kwanza tu za 2026, zaidi ya watu 40 wamefariki barabarani.

“Mpango huu ni sehemu ya mkakati wetu mpana wa usalama barabarani. Uendeshaji salama huanza na uwezo wa dereva kuona vizuri. Kwa kutambua na kurekebisha masuala ya kuona, tunatumai kupunguza vifo barabarani na majeraha” NTSA ilisema.

Mamlaka hiyo imeipa kipaumbele Nairobi kutokana na idadi kubwa ya magari na viwango vya ajali lakini inapanga kuzindua mpango huo kote nchini katika miezi ijayo.