Makala

Yummy Mummy afichua alivyoacha kazi nzuri kuokoa ndoa yake

March 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA SINDA MATIKO

MWANAPODKASTA na mtengenezaji maudhui maarufu Murugi Munyi amefichua kuwa ndoa yake ndiyo ilimfanya kuacha kazi ya kishua katika kampuni ya Sportpesa.

Munyi almaarufu kama Yummy Mummy, alijiunga na Sportpesa kutoka kampuni ya RedHouse iliyojihusisha zaidi na masuala ya mawasiliano.

“Pale RedHouse mshahara ulikuwa mzuri nilikuwa napokea Sh200, 000 halafu nilikuwa na mume ambaye naye alikuwa analipwa vizuri. Sema sikukaa sana, baada ya mwaka na nusu nikaondoka na kujiunga na Sportpesa,” Munyi anasema.
Pale Sportpesa mshahara wake uliboreka hata zaidi.

“Sportpesa nilikuwa afisa mkuu wa mawasiliano na mshahara ulikuwa mkubwa hata zaidi. Nilikuwa napokea Sh350, 000 kila mwezi lakini kizuri hata zaidi ni kwamba kila baada ya miezi mitatu waajiriwa wa Sportpesa tulikuwa tunalipwa mshahara maradufu,”
Baada ya mwaka na miezi kadhaa, Munyi aligura tena na kujiunga na kampuni ya My Dawa kusimamia mawasiliano.

“Mshahara wa Sportpesa ulikuwa mzuri kwa kweli lakini sababu za mimi kuondoka wala haikuhusiana kabisa na maslahi. Ilikuwa ni kipindi ambacho ndoa yangu ilikuwa kwenye msukosuko hivyo ikanilazimu niwache kazi niipambanie. Mimi ni baadhi ya watu ambao utendaji wetu huadhiriwa zaidi na hisia za moyoni. Singeweza kufanya kazi vizuri wakati ndoa yangu ikiwa inapumulia mashine,” anasema.
Munyi alikuwa akirejelea sakata ya mchepuko iliyogonga vichwa vya habari. Mume wa Munyi alianza kuchepuka na nesi mmoja maarufu, hii ikiwa ni baada yake kugundua kuwa mke wake naye alikuwa akimchepukia.

Msukosuko huo ulitishia kuvuruga ndoa mbili na ndicho kipindi Munyi anasema alilazimika kuacha kazi ya maana kuipambania ndoa yake.

Baada ya kufanikiwa kuikoa ndoa yake, Munyi alijiunga na kampuni ya My Dawa ambapo anasema hakukaa zaidi ya mwaka.

“Mshahara pale My Dawa pia ulikuwa mzuri nikiwa kama meneja wa mawawilisiliano ila nilishindwa kudumu maaana mimi na bosi wangu hatukuwa tunapikika kwenye chungu kimoja. Lakini pia ilikuwa kipindi ambacho taaluma yangu kama mtengenezaji maudhui kilikuwa kimeanza kushika kasi. Hapo ndipo nilifanya uamuzi wa kuachana na kazi ya kuajiriwa ili kujikita zaidi kwenye utengenezaji wa maudhui. Nakumbuka baada ya kulamba dili yangu ya kwanza ya Sh100, 000 nikawa na kichocheo zaidi cha kuendelea.”