Makala

Zawadi ya Ruto kwa masikini 2.2 milioni kuhusu afya

Na  MERCY CHELANGAT, BENSON MATHEKA September 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Rais William Ruto ameanzisha rasmi mpango wa serikali wa kufadhili huduma za afya kwa watu wasioweza kujilipia, ambapo familia 558,000 zilizo na jumla ya watu milioni 2.2 zitanufaika kupitia Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA).

Akizungumza katika Ikulu ya Nairobi, Rais Ruto alisema kuwa huduma za matibabu ya wasiolazwa katika zahanati, vituo vya afya, na hospitali za kaunti ndogo sasa zitakuwa bila malipo kwa Wakenya wote.

“Wapo Wakenya wanaolipa kati ya Sh1,020 hadi Sh1,500 kwa mwezi. Lakini tunafahamu wapo ambao hawawezi kulipa hata Sh300. Kwa hivyo, serikali italipia kundi hili. Huu ndio usawa na haki unaotajwa na Katiba yetu,” alisema Rais.

Rais alisisitiza kuwa hakuna Mkenya anayestahili kukosa matibabu kwa sababu ya ukosefu wa fedha. Alisema kuwa kila mgonjwa anatakiwa kuhudumiwa, kupewa dawa, na kuruhusiwa kwenda nyumbani bila kulipa chochote.

Aidha, alitangaza kuwa serikali itanunua vifaa vya matibabu vya thamani ya Sh220 bilioni kwa  hospitali za kaunti zote 47, ambapo kaunti 25 tayari zimepokea vifaa hivyo  na huduma za matibabu pia zitakuwa za dijitali katika hospitali za ngazi ya 2 na 3 ifikapo Novemba.

Mpango huu unatekelezwa chini ya Sheria ya Bima ya Afya ya Jamii ya 2023 na kanuni zake za 2024. Rais Ruto alihimiza wabunge kutumia Hazina ya Maendeleo ya Maeneobunge (NG-CDF) kusaidia kugharamia wananchi wasiojiweza.

Kufikia sasa, zaidi ya Wakenya milioni 26 wamesajiliwa na SHA, huku milioni 5.5 wakipokea huduma za afya. Mamlaka hiyo imekusanya Sh70 bilioni kutoka kwa wachangiaji milioni 4.8.

Waziri wa Afya Aden Duale alisema kuwa Bunge liliidhinisha Sh13 bilioni  kwa afya ya msingi mwaka huu, na magavana wameahidi kuchangia kati ya Sh15,000 hadi Sh50,000 kwa kila familia isiyojiweza katika kaunti zao.

Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga, kwa niaba ya Baraza la Magavana, aliunga mkono mpango huo akisema utafaidi zaidi ya Wakenya milioni 12 wanaoishi katika umasikini. Hata hivyo, alionya kuwa Kenya iko hatarini kukosa kufikia malengo ya SDG kuhusu vifo vya akina mama wajawazito kufikia mwaka 2030.

Aliitaka Wizara ya Afya kuondoa marufuku ya hospitali za kiwango cha 2 kutotoa huduma za kujifungua, kwani ndio vituo vinavyofikiwa zaidi vijijini.

Dkt Dennis Miskellah wa chama cha madaktari (KMPDU), alisema kuwa Rais aliahidi kuajiri wahudumu wa afya 7,000 kwa mikataba ya kudumu, kama sehemu ya mpango wa kuimarisha UHC. Alieleza kuwa serikali itashirikiana na magavana kupanga ajira ya kila mwaka ya wahudumu wa afya, kama inavyofanyika kwa polisi na wanajeshi.

Hata hivyo, baadhi ya watoa huduma binafsi, kama vile Brian Lishenga wa chama cha hospitali binafsi (Rupha), walikosoa mpango huo wakisema hauna msingi thabiti wa kisheria na si endelevu kifedha.