Michezo

Mane asema hataki majukumu ya kupiga penalti

July 6th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

NYOTA wa Senegal na klabu ya Liverpool, Sadio Mane, ameamua kuacha kupigia Teranga Lions penalti baada ya kupoteza mbili kwenye Kombe la Afrika (AFCON) linaloendelea nchini Misri.

Mshambuliaji huyu, ambaye aliibuka mfungaji bora kwenye Ligi Kuu ya Uingereza ya msimu 2018-2019 kwa mabao 22 kwa pamoja na mchezaji mwenza Mohamed Salah na raia wa Gabon, Pierre-Emerick Aubameyang wa Arsenal, alipoteza penalti yake ya kwanza dhidi ya Harambee Stars ya Kenya mnamo Julai 1.

Kipa Patrick Matasi alipangua penalti ya Mane, ambaye hata hivyo ilijiondolea aibu kwa kufuma wavuni penalti nyingine baadaye pamoja na bao lingine Senegal ikizamisha vijana wa kocha Sebastien Migne kwa mabao 3-0 katika mechi ya mwisho ya Kundi C.

Mane, ambaye amewahi kuwa katika orodha ya wachezaji tatu-bora kwenye tuzo za mwanasoka bora wa Afrika mwaka 2016, 2017 na 2018, alipoteza penalti nyingine dhidi ya Uganda Cranes katika mechi ya raundi ya 16-bora hapo Julai 5.

Mchezaji huyu anayefahamika kwa kasi ya kutisha na makombora mazito alichezewa visivyo na kipa Denis Onyango ambaye alimpa kila sababu ya kuamua kuachana na upigaji wa penalti baada ya kumzima tena.

Hata hivyo, Mane alipachika bao la ushindi baada ya Senegal kuiba pasi ya Godfrey Walusimbi na kumegeana pasi za haraka haraka kabla ya Mane kumalizia shambulio hilo kwa ustadi.

‘Sitaki’

Tovuti ya Ghana Soccernet sasa inasema kuwa Mane, ambaye anaongoza jedwali la wafungaji wa mabao nchini Misri, ameamua hataki kupiga penalti za timu ya taifa.

“Sitaki kuwa mchoyo kupiga kila penalti,” alisema Mane kabla ya kuongeza, “Nitaacha kupiga penalti baada ya kupoteza mbili kufikia sasa katika mashindano haya.”

“Naweka timu yangu mbele kwanza, na nitapatia mchezaji mwingine fursa ya tukipata penalti katika mechi zijazo.”

Itakumbukwa pia Mane alipoteza penalti katika AFCON miaka miwili iliyopita nchini Gabon.