Maoni

Adhabu ya TSC dhidi ya walimu wa JSS itadhuru shule za umma

June 14th, 2024 2 min read

NA MARY WANGARI

TUME ya Kuwaajiri Walimu nchini (TSC) mapema wiki hii iliwapiga kalamu walimu kadhaa wa Sekondari ya Msingi (JSS) siku mbili tu baada ya kusitisha mgomo wao.

Hatua hiyo ilijiri siku chache tu baada ya Bunge la Kitaifa kupitisha bajeti mpya ya Sh4.006 trilioni ambayo ndiyo kubwa zaidi katika historia ya Kenya.

Katika bajeti hiyo, Wabunge waliafikiana kuhusu mgao wa Sh28.88 bilioni katika bajeti mpya ya 2024/2025, ili kufanikisha ajira ya kudumu kwa walimu 46,000 wa JSS.

Kiasi hicho cha pesa kinajumuisha Sh8.3 bilioni zitakazotumika kuajiri kundi la kwanza la walimu 26,000 huku Sh 4.68 bilioni zikitumika kuwaajiri walimu 20,000 kuanzia Julai 1, kinyume na mpango wa awali wa TSC kuhusu kuwaajiri walimu wa JSS kuanzia Januari 1, 2025.

Huku suala tata kuhusu ajira likionekana kutatuliwa, wasiwasi umezuka kwamba hali ya vuta nikuvute inayojitokeza katika JSS huenda ikazidisha pengo kati ya wanafunzi kutoka familia maskini na walio matajiri.

Isitoshe, hatua ya TSC kuwafuta kazi walimu hao wanagenzi siku chache baada ya kusitisha mgomo wao itaathiri shule za sekondari msingi za umma.
Licha ya kuwepo malalamishi kuhusu ukosefu wa miundomsingi na vifaa muhimu vya kufanikisha CBC katika shule za msingi, Wizara ya Elimu imeshikilia msimamo wake kuhusu kudumisha wanafunzi wa JSS katika shule za sekondari.

Akizungumza Aprili, Katibu wa Wizara ya Elimu Belio Kipsang alipuuzilia mbali uwezekano wowote wa kuhamisha wanafunzi wa Gredi ya 9, katika shule za sekondari akisema hakuna muda wa kutosha.

Akitetea uamuzi huo, alisema uamuzi huo unawiana na maoni ya wadau wa elimu yaliyokusanywa na Jopokazi la Afisi ya Rais kuhusu Mageuzi ya Elimu na pia uliungwa mkono sehemu kubwa ya Wakenya.

Hata hivyo, kadri siku zinavyosonga, masuala nyeti yamezidi kujitokeza kuhusu changamoto zinazokumba JSS na kuibua hisia mseto miongoni mwa wazazi na walezi.

Kando na mivutano inayogubika utekelezaji wa CBC, kuna wasiwasi kwamba wanafunzi wa JSS kutoka familia maskini huenda wakafungiwa nje ya baadhi ya kozi hususan Sayansi, Teknolojia na Hisabati (STEM).

Idadi kubwa ya wanafunzi kutoka jamii maskini wasioweza kumudu shule za kibinafsi, wamelazimika kusomea shule za msingi za umma zinazokabiliwa na matatizo mengi.

Shule nyingi za umma hasa katika maeneo ya mashinani hazina stima, intaneti, maabara na miundomsingi muhimu inayohitajika hasa katika masomo ya STEM.

Hali ni tofauti kabisa na wanafunzi ambao familia zao zinaweza kumudu shule za kibinafsi zilizo na miundomsingi bora zaidi ikizingatiwa sehemu kubwa zimetimiza masharti makali yaliyowekwa.

mwnyambura@ke.nationmedia.com