Huenda bodaboda wakageuka janga iwapo hawatadhibitiwa kisheria
TUKIO la hivi majuzi ambapo waendeshaji bodaboda waliteketeza basi eneo la Donholm, Nairobi, limezua hisia mseto na wasiwasi kuhusu tabia ya uhuni na kuchukua sheria mikononi, hasa katika sekta ya bodaboda.
Inahuzunisha kwamba mwendeshaji bodaboda alipoteza maisha yake kwenye mkasa huo.
Hata hivyo, maswali mengi yamezuka kuhusiana na tukio hilo, mojawapo likiwa; je ingalikuwa vipi kama ni mpita-njia angegongwa na kulemazwa au kuuawa na mwendeshaji bodaboda?
Raia wangalikuwa na haki ya kumwadhibu mhusika kwa kuteketeza pikipiki ambayo ama ni yake binafsi au ameajiriwa kuitumia kuchuma riziki?
Vipi kuhusu waendeshaji magari? Wana haki ya kuungana na kuwaadhibu waendeshaji bodaboda wanaosababisha ajali kwa kukiuka sheria za trafiki kimaksudi?
Si mara ya kwanza waendeshaji bodaboda wameungana na kuteketeza gari au hata gari pamoja na dereva, baada ya ajali kufanyika.
Wapita-njia vilevile hawajanusurika, huku wengi wakiachwa waking’ang’ana kugharimia matibabu, kugeuzwa vilema na hata kupoteza maisha baada ya kuangushwa au kugongwa na bodaboda.
Uhalisia wa kero la waendeshaji bodaboda unajitokeza bayana maeneo ya mijini, ambapo ni kana kwamba sekta hii ina sheria zake mahsusi inazofuata, tofauti kabisa na Wakenya wengine.
Kwa hakika, njia moja ya kugeuka kilema au kuangamia upesi zaidi mijini ni kupitia ama kuabiri au kugongwa na bodaboda.
Kuanzia kupuuza ishara na sheria za trafiki, kupita mikondo isiyofaa barabarani, kupita sehemu zilizotengewa watembea kwa miguu, kufunga mapito ya umma kwa kuegesha pikipiki kiholela nje ya maduka na sehemu nyinginezo kinyume na sheria, ni baadhi tu ya masaibu yanayowakumba Wakenya wanaofanya kazi au biashara jijini.
Sikuelezi kuhusu matusi wanayomiminiwa wahasiriwa wanaonusurika kugongwa na bodaboda.
Kwenye kilele cha maandamano ya Gen-Z, video kadhaa zilizosambazwa mno mitandaoni zilionyesha majambazi waliotumia pikipiki walivyowahangaisha Wakenya mitaani, Nairobi, kwa kuwashambulia na kuwapora mchana peupe kabla ya kutoweka wakitumia bodaboda.
Licha ya kuwepo kwa sheria za kudhibiti bodaboda, ikiwemo marufuku ya kuendesha shughuli zao katika maeneo fulani ya jiji kuu, ni wazi kuwa zimesalia nakala tu, huku sekta hii ikiachwa huru kufanya inavyotaka.
Hali kwamba bodaboda hutumika sana kisiasa, hasa kwenye kampeni, imechangia kero hili.
Waendeshaji bodaboda hawako juu ya sheria; sawia na Wakenya wote, wawe ni wapita-njia, wanaovuta mikokoteni au waendeshaji magari.
Katiba inawahakikishia haki na uhuru raia wote, lakini uhuru huu ni sharti uambatane na uwajibikaji. Wakati wote, uhuru usio na kipimo ni hatari.
Wahudumu wa bodaboda ni sharti wadhibitiwe kabla ya kugeuka janga lisiloweza kudhibitiwa.