Maoni

Kenya pia ibuni mpango wa kuokoa raia wake Sudan Kusini

Na DOUGLAS MUTUA March 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SINA hakika kiongozi wa majeshi ya Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ana akili timamu, lakini ninafurahia anavyotutobolea siri za nchi yake mtandaoni.

Juzi amejigamba jinsi alivyowapeleka wanajeshi wake nchini Sudan Kusini ili kulinda maslahi ya Uganda na kumsaidia Rais Salva Kiir kudumu mamlakani.

Kisa na maana ni kwamba Rais Kiir na makamu wake, Dkt Riek Machar, wamekosana tena kwa mara ya ngapi … sijui, na huenda Sudan Kusini kukatokea vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Rais Kiir – anayeongoza serikali ya muungano kati yake, Dkt Machar na makundi mengineyo – amewafukuza kazi na kuwakamata baadhi ya washirika wa makamu wake huyo, hatua ambayo imeleta hali ya taharuki nchini humo.

Ikizingatiwa kwamba Uganda imewahi kuwapeleka wanajeshi wake Sudan Kusini mara kadhaa, na wakati mmoja wakauawa zaidi ya 50 kwa siku moja, inabidi tujiulize ina maslahi gani ambayo inalinda huko.

Swali jingine la kujiuliza ni iwapo Kenya ina maslahi yoyote Sudan Kusini, hasa kwa kuwa imejitia hamnazo taharuki hiyo kana kwamba vita vikizuka havitaiathiri kwa vyovyote.

Ikiwa kuna nchi ambayo inapaswa kujali kuhusu maslahi yake nchini Sudan Kusini kwa wakati huu ni Kenya. Makuzi ya taifa hilo changa yanategemea zaidi utulivu nchini Kenya kwa kuwa miamala yake mikuu ya kibiashara hufanyiwa Nairobi.

Viongozi wengi wakuu wa serikali na hata waasi wana nyumba nchini Kenya, wameficha familia zao Nairobi, au hata wanaendesha biashara zao halali na haramu nchini mwetu.

Maelfu ya Wasudan Kusini wanaishi kwenye miji kadha ya Kenya, watoto wao wanasoma shule zetu, na kwa jumla idadi hiyo kubwa ya watu haijaonyesha dalili kwamba inatamani kurejea Juba.

Wapo Wakenya wengi wanaoishi katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba, kwa hivyo tunategemeana kikazi na kibiashara.

Tusipofanya biashara na taifa hilo, basi halikui kiuchumi wala kiutawala na kuwa taifa la kisasa.

Kutokana na utulivu wa kadri ulio nchini Kenya, inatabirika kwamba vita vikizuka Sudan Kusini, wakimbizi watamiminika nchini Kenya na kuketi huku mpaka hali ya utulivu irejee, warudi nyumbani au waamue kuwa wananchi wa kimataifa kabisa.

Mtagusano huo, sikwambii na kuzaliana si haba, unapaswa kuwapa majasusi wa kimataifa kibarua cha kujikuna kichwa pale amani ya taifa moja au yote mawili inapotishiwa.

Tusidanganyane: Juba kukiwaka moto, raia watakimbilia Kenya kwanza hata kabla ya kuwaza kuhusu taifa linaloitwa Uganda.

Nairobi ndio mji bora eneo la Afrika Mashariki, kwa hivyo kila anayepata mitihani ya maisha hujaribu kutafuta afueni huko.

Singeshangaa ningesikia kwamba majeshi ya Kenya yamefika Juba ghafla ili kudhibiti hali; singeshangaa wala kuwazia kutofika huko kwa majeshi ya Uganda.

Kimsingi, katika hali ya kawaida, maslahi ya Kenya nchini Sudan Kusini ni mengi na mapana kuliko ya Uganda. Japo mataifa yote matatu yanapakana, Kenya ni chaguo bora kuliko Uganda.

Huwezi kulinganisha Nairobi na Kampala. Kamwe! Hata hivyo, wizi wa rasilmali za asili ambao Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda na mwanawe, Jenerali Muhoozi, wanaendeleza kule wakisaidiwa na Rais Kiir hauwaruhusu kutulia Uganda.

Mtiririko wa mafuta, migodi ya dhahabu na madini mengineyo kutoka Sudan Kusini ukitishiwa, madikteta hao watatu wanaingia kiwewe na kufanya kila wawezalo ili utawala usalie ule-ule, waendelee na biashara yao haramu.

Kwa kuwa maslahi ya Kenya ni tofauti na hayo ya wizi wa mali za watu, Serikali yetu inapaswa kuwapeleka wanajeshi wa ulinzi wa taifa (KDF) nchini Sudan Kusini kwa ajili ya kuwalinda, na ikibidi kuwarejesha nyumbani, Wakenya wanaoishi huko.

Hakuna Mkenya anayepaswa kufia huko kwa kuwa tumezembea. Tumejua mapema maisha yao yamo hatarini. Hatupaswi kuwaona wakilia ‘Serikali saidia’ wakati ambapo Juba hakufikiki kutokana na vita.