Maoni

Kuna ukweli kwa aliyosema Gachagua, viongozi wa Kaskazini Mashariki wamakinikie maendeleo

Na CECIL ODONGO January 12th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

WIKI jana aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua alizua cheche kali kwa kudai kwamba baadhi ya maeneo hayajashuhudia maendeleo makubwa nchini tangu mfumo wa ugatuzi uanzishwe kutokana na matumizi mabaya ya fedha.

Kauli yake ilichochewa na miundomsingi duni hasa katika Ukanda wa Kaskazini Mashariki, eneo ambalo halionekani kupiga hatua kimaendeleo licha ya kwamba lilibaguliwa sana kabla ya mfumo wa kugatua na kusambaza rasilimali mashinani kukumbatiwa 2013.

Matamshi hayo ya Bw Gachagua yalitokana na malalamishi kwamba wanafunzi kutoka maeneo mengine kwa mfano kaskazini mwa nchi huja kusomea shule za kitaifa zinazopatikana Mlima Kenya na kuwafungia nje wenyeji.

Kwa ufupi Bw Gachagua alikuwa akiwaambia viongozi wa Kaskazini mwa Kenya watumie rasilimali zilizotengewa eneo lao kuliimarisha ili hata wanafunzi wa maeneo mengine ya nchi nao pia wanufaike miundomsingi ya Kaskazini mwa Kenya.

Mwanzo, suala hili huenda likawa na mtazamo wa kisiasa ila kwa kiasi fulani pia lina ukweli wake.

Tangu 2013, Kaunti ya Mandera imepokea Sh111.8 bilioni, Wajir (Sh94.1 bilioni), Garissa (Sh80.4 bilioni) kisha Marsabit Sh76.83 bilioni).

Katika mwaka huu wa kifedha wa 2025/26, Garissa imepokea Sh8.7 bilioni, Wajir (Sh10.3 bilioni), Mandera (Sh12.2 bilioni) na Marsabit Sh7.9 bilioni.

Mgao wote huu angalau ungesaidia kubadilisha kaskazini mashariki kiuchumi na kimaendeleo lakini bado ni eneo ambalo lina viwango vya juu vya umaskini, zaidi ya miaka 10 baada ya ugatuzi kuanza.

Kwa hili huenda kauli ya Bw Gachagua inaafiki na wanasiasa wa eneo hili wanastahili kuzinduka usingizini ili kutumia vyema mgao kutoka Hazina Kuu ya Kifedha.

Mfumo ambao umekuwa ukitumiwa kuamua kaunti hupokea pesa ngapi kila mwaka wa kifedha, umekuwa ukipendelea kaunti za kaskazini mashariki ndiyo maana hakuna sababu za kaunti hizo bado kusalia nyuma kimaendeleo.

Hii ni kwa sababu mfumo huo umekuwa ukizingatia sana ukubwa wa eneo badala ya wingi wa watu.

Mnamo Januari 3, 2019 aliyekuwa Gavana wa Mandera Ali Roba (sasa seneta) aliwaongoza wabunge na viongozi kutoka kaskazini mwa Kenya kupinga fomyula mpya iliyokuwa imependekezwa kutoa mgao wa fedha kwa kaunti.

Walidai kuwa eneo hilo lingepoteza Sh10 bilioni kila mwaka iwapo fomyula hiyo mpya ingekumbatiwa.

Kwa kifupi Bw Roba na wenzake hawakuwa wakitaka wingi wa watu utumike kama kigezo cha kuongezea kaunti nyingine hela na kuzipunguzia magatuzi yao.

Hadi sasa Mandera, Turkana na kaunti nyingine za kaskazini mwa Kenya zinapokea mgao mkubwa kutoka Hazina Kuu ya Kifedha kwa kuzingatia ukubwa wao.

Kama tu kaunti nyingine nchini, ripoti ya Mkaguzi wa Bajeti ya Serikali imekuwa ikianika matumizi mabaya ya fedha na ufisadi eneo la kaskazini mashariki.

Ni jukumu la viongozi hasa magavana wa maeneo hayo kujizatiti na kufikisha miradi ya maendeleo kwa raia ili kudhihirisha kuwa ugatuzi unathaminiwa na umebadilisha maisha ya wengi.

Afadhali kuwe na mabadiliko katika maisha ya raia kaskazini mashariki hata kidogo badala ya kaunti kuendelea kupata pesa na zinaishia mishahara au kutumika vibaya kwenye masuala yasiyonufaisha raia.

Miradi ya maji, uimarishaji miundomsingi, elimu, ufugaji na afya ni kati malengo ya maendeleo ambayo yatawasaidia wakazi wa kaskazini mashariki ambao kitega uchumi kwao ni ufugaji wa kuhamahama.