Maoni

Kuondoa upigaji msasa katika mchakato wa kutoa vitambulisho ni hatari

April 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA JURGEN NAMBEKA

HATUA ya Rais William Ruto kutangaza kuondolewa kwa utaratibu wa kupiga msasa vijana wanaotafuta vitambulisho kuanzia Mei, ni ishara nzuri kwa jamii mbalimbali zilizokuwa zikibaguliwa katika shughuli hiyo.

Kwa Waislamu na pia jamii zingine kama vile Wabajuni, Wasomali na kadhalika, shughuli hiyo ya kupata vitambulisho ilikuwa ni mahangaiko tele.

Hivyo kuondolewa kwa kupigwa msasa huenda kukapunguza ubaguzi dhidi yao na kuchangia kwa usawa wakati wa shughuli hiyo.

Aidha, kuondoa kwa upigwaji msasa pia kutarahisisha mchakato wa kutafuta vitambulisho kwa Waislamu na jamii zilizotengwa, na kuwasaidia kupata huduma muhimu na hata kupiga kura.

Sera hii inapopitishwa, kumekuwa na malalamishi mitandaoni Wakenya wakieleza kuwa, kuondolewa kwa hatua hiyo kwenye mchakato mzima huenda kukawahatarisha maisha ya Wakenya.

Hii ni licha ya Rais Ruto kueleza kuwa hawatalegeza kamba kwa upande wa usalama hata hilo linapofanyika.

Wakenya kadhaa walieleza kuwa, kuondolewa kwa hatua hiyo kunaweza kuleta athari za kiusalama, watu wakipata vitambulisho kwa njia rahisi na kuzitumia kutekeleza maovu.

Isitoshe, kuna uwezekano wa watu kutumia stakabadhi zisizo za kweli kupata vitambulisho na kuenda kinyume na uadilifu wa mfumo wa kuwatambua Wakenya.

Pia, huenda ikahitilafiana na usahihi wa data za Wakenya. Kuondolea kwa sehemu hiyo ya mchakato huenda ikaibua masuala ya usahihi ambao utahitilafiana na rekodi kamili na kuwa na athari za kisheria au kiutawala.

Ni muhimu kuwazia pia athari zinazoweza kuambatana na hatua ya kutochunguza historia ya baadhi ya wanaosaka hati hizo muhimu za kitaifa.