Kushambuliwa hakutazuia shirika la NMG kutekeleza wajibu wake wa kutoa habari kwa umma
KATIKA siku za hivi karibuni, taifa limeshuhudia kampeni ya chuki na potovu, iliyopangwa na yenye nia mbaya mitandaoni dhidi ya shirika la habari la Nation Media Group.
Iwapo waendeshaji kampeni hiyo potovu wa kulipwa wangekuwa na uwezo, NMG ingekuwa imekufa na ‘iliyolala salama’. #RIPNationMedia ndio heshitegi ya hivi punde zaidi kutumiwa na wanapropaganda kwenye krusedi za kupotosha dhidi ya Nation kwenye mtandao wa X (awali Twitter).
Wanapropaganda hao Ijumaa waliandika barua feki iliyodai kwamba takriban wafanyakazi 600 wa NMG watafutwa kazi kufikia Aprili mwaka huu. Kisha wakalipa makundi ya watu mitandaoni kusambaza jumbe za chuki zingine zikiwa na video za viongozi wa ngazi za juu wa serikali iliyoko mamlakani ambao walitoa matamshi hadharani ya kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari. Ni rahisi sana kuona mpango huo wa kioga.
Wimbi la sasa la kusambaza habari za kupotosha lilianza Jumanne, Januari 30, 2024. Ni vigumu kukosa kuona sadfa kwamba hiyo ilikuwa siku ambapo Nation ilizindua kipindi cha “Broken System”, ambacho kinaangazia jinsi utoaji huduma msingi za serikali ulivyodorora kupitia kufanya mahojiano na Wakenya wa kawaida kueleza wanayopitia kila siku mikononi mwa maafisa wa kutoa huduma za serikali.
Kipindi cha kwanza kwenye mtiririko wa Broken System kiliangazia mahangaiko ya wagonjwa katika hospitali kuu ya rufaa nchini, KNH.
Kilionyesha mateso na maafa yanayotokea kila siku kwenye vibaraza vya KNH, yakiandama zaidi wananchi ambao hawawezi kumudu ada ghali za hospitali za kibinafsi.
Wanahabari wetu pia walitembelea afisi za utoaji paspoti za Wizara ya Mambo ya Ndani na kuelezea mahangaiko yasiyomithilika ya Wakenya wanaotafuta stakabadhi hiyo muhimu.
Katika Bima House, wanahabari wetu walishuhudia mashaka ya wazee wanaofuatilia malipo yao ya uzeeni huku maafisa wa serikali wakiwahangaisha kwa nia ya kutafuta kuhongwa.
Katika kipindi cha pili kilichochapishwa Jumanne ya Februari 6, kiliangazia mateso ya Wakenya zaidi ya 600,000 ambao wamekuwa wakisubiri kupata vitambulisho vyao vya kitaifa tangu Novemba, bila hakikisho lolote kuhusu lini watapokea stakabadhi hiyo muhimu mno.
Soma: Jasho kupata kitambulisho, umepitia yapi kusaka stakabadhi hii?
Kama shirika lililo na uwajibikaji, NMG ilitafuta maoni kutoka kwa viongozi wa serikali wanaosimamia mashirika ambayo yaliangaziwa na usemi wao ulijumuishwa vyema kwenye machapisho.
Zaidi ya hayo, wanahabari wa NMG walichukua muda wao kueleza visiki ambavyo viko nje ya uwezo wa serikali ambavyo huenda vinachangia tatizo hilo.
Katika stori ya kucheleweshwa kwa vitambulisho vya kitaifa, kwa mfano, ilieleza jinsi agizo la mahakama kuhusu kusimamishwa kwa uchapishaji wa vitambulisho aina ya ‘third generation’ lilikuwa limesababisha kuchelewa kwa vitambulisho hivyo.
Mnamo Jumanne wiki hii, barua feki ilichapishwa kwenye X ikidai kwamba wino ambao unatumiwa kuchapisha magazeti ya Nation unaweza kuwa na athari mbaya za kiafya kwa wasomaji.
Shirika la ukadiriaji wa ubora wa bidhaa (Kebs) lilitangaza kwamba halikuhusika na taarifa hiyo, lakini hii ilifanyika baada ya barua hiyo feki kusambazwa mara nyingi na watumiaji wa mitandao.
La kushangaza, baadhi ya watu waliodai kwamba ni maafisa wa Kebs walitembelea afisi zetu za uchapishaji zilizoko Mombasa Road, wakitaka “kukagua ubora wa wino wetu.”
Mtindo wa kushambulia NMG bila msingi wowote kama shirika na pia wanahabari binafsi haushangazi tu bali pia hauwezi kukubalika.
NMG wakati wote hukubali kukaguliwa na hukubali ukosoaji wa uanahabari wake. Nation ndilo shirika la pekee la habari nchini ambalo limeajiri Mhariri wa kukusanya maoni na malalamishi ya umma.
Pale mahali ambapo tumekosa kufikia vigezo vyetu vya hali ya juu, huwa hatusiti kuchapisha marekebisho, mafafanuzi na maombi ya radhi kama hali inavyohitaji.
Baraza la Uanahabari nchini (MCK) pia ni shirika ambalo wanaohisi kukosewa na utangazaji wetu wanaweza kupeleka kesi zao huko ili zitatuliwe. Pia, mahakama katika miaka mingi imefanya maamuzi makubwa dhidi au kuunga mkono uanahabari wetu.
Hii, bila shaka ni idhibati tosha kwamba hakuna uhaba wa mianya ya kuelezea kutoridhika kwa mtu dhidi ya machapisho ya Nation Media Group.
Wimbi la sasa la chuki dhidi ya NMG halijatoa nafasi kwa shirika hili kujadiliana na wanaodaiwa kukosewa na machapisho yetu katika njia ya kingwana kama inavyotarajiwa kupitia demokrasia ya taifa letu huru.
NMG kama shirika lililo na imani nzito katika utawala wa kisheria, limeripoti visa hivi kwa kitengo cha upelelezi wa jinai (DCI) pamoja na kuwasilisha malalamishi kwa wamiliki wa mtandao wa X (Twitter).
Ni matumaini yetu kwamba DCI itachunguza na kuchukulia hatua wasambazaji wa jumbe za chuki na za kupotosha dhidi ya NMG.
Tumeelezea pia kwa bayana kwa X kwamba mtandao wao unatumiwa kusambaza uongo na chuki dhidi ya shirika halali la habari.
Kwa miongo sita na nusu sasa, NMG imekuwa ikifuatilia habari zinazomhusu mwananchi wa kawaida kwa nia bayana ya kuwezesha jamii kwa njia bora.
Tunahakikishia wasomaji na watazamaji wetu wote kwamba tutaendelea na misheni hii.