Maoni

MAONI: Lala penye wema Raila, Rais tuliyenyimwa na uovu wetu

Na DOUGLAS MUTUA October 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

NA IWE RASMI SASA: mwamba aliyefariki hivi majuzi ndiye aliyeshinda uchaguzi wa urais wa 2007.

Raila Amollo Odinga hakuwa kinara wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) tu, wala mgombea wa urais wa miungano mingine ya kisiasa baada ya hapo, bali pia rais tuliyenyimwa na uovu wetu wenyewe.

Ujumbe wangu kwa Wakenya wanaojuta na kusema Raila angalichaguliwa rais katika uchaguzi wa mwaka 2022, aliyekuwa mgombea mwenziwe, Bi Martha Karua, angalikuwa rais leo, ni kwamba Mungu si mjinga!

Bi Karua ni mmoja wa waliompokonya Raila ushindi katika uchaguzi wa 2007, hivyo hapaswi kufaidika mara mbili, wizi wa kura za Raila na kifo chake vilevile. Kwamba, baadaye waliridhiana si hoja; Kenya ilipata doa kutokana na wizi huo.

Wakati huo niliripotia magazeti haya, na kamwe sijasahau kiburi na jeuri ya walioiba ushindi wa Raila na kumuapisha Rais Mwai Kibaki usiku wa kiza.

Ni rahisi kusema tusahau yaliyopita, lakini ni muhimu kusahihisha mambo na kuiweka sawa historia.

Kwa waliompenda na kumuenzi Raila, makiwa. Wingu jeusi lililojifanyia utando juu yenu litaondoka; itakucha siku njema.

Kwa waliomchukia na kumbeza wakati wote, mmepoteza tunu msiyoitambua, ila iliyowaweka salama kwa kuwaogofya watesi wenu.

Asingalikuwapo duniani, labda mngalipotezwa msiwahi kupatikana tena! Kenya imetokwa na mzalendo.

Kifo chake kinanikumbudsha kile cha Daniel Moi, aliyeiongoza Kenya kwa miaka 24 hadi 2002.

Si siri kwamba baadhi yetu tuliozaliwa na kulelewa katika mazingira ya hofu enzi Moi akiwika kama jogoo hatukumsamehe hadi alipofariki 2020.

Tuliamini kwa dhati ya nyoyo zetu kwamba, mikono ya Moi ilijaa damu za watu wengi waliouawa wakati wa utawala wake: wanasiasa, wanaharakati, wanafunzi, na wengineo.

Tuliamini alistahili kuondoka na kusahaulika kabisa. Binafsi nilimsamehe kutokana na ujumbe ulioandikwa na kupakiwa kwenye mitandao ya kijamii na rafiki yangu, Dkt. Ezekiel Mutua, aliyekuwa afisa mkuu mtendaji wa halmashauri ya udhibiti wa filamu nchini.

Dkt Mutua aliuliza: “Ikiwa bado hujamsamehe Rais Moi, karibu miaka 20 tangu aondoke mamlakani kwa hiari, unapaswa kuuchunguza moyo wako, ujiulize iwapo tatizo lilikuwa Moi, au wewe mwenyewe.”

Nawatolea mfano huu watu ambao huenda bado wana kinyongo na marehemu Raila, pengine kutokana na maamuzi yake ya kisiasa ambayo hayakuwaridhisha.

Hakika, mfano wenyewe hauafiki kikamilifu kwa kuwa mikono ya Raila ni safi kama pamba.

Ameondoka na jina lake zuri kwa sababu moja kuu: Ndiye mwanasiasa pekee wa ngazi yake ambaye ameaga dunia bila tuhuma za kuua!

[email protected]