MAONI: Anayetaka kumrithi Raila awe jasiri na mtetezi sugu wa raia
SIASA za urithi wa kiongozi wa Azimio la Umoja One Kenya zimeanza kushuhudiwa katika nyanja tatu tofauti, ndani ya muungano huo, katika chama chake cha ODM na katika ngome yake ya kisiasa ya Nyanza.
Hii ni baada ya mwanasiasa huyo mkongwe kutangaza azma ya kuwania wadhifa wa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), ishara kuwa analenga kujiondoa katika ulingo wa siasa za humu nchini.
Katika Azimio, mienendeo na semi za kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka zinaashiria kuwa anajizatiti kuvalia kiatu kikubwa cha Bw Odinga.
Ndani ya majuma mawili yaliyopita, Bw Musyoka ameongoza mikutano miwili ya vinara wakuu wa muungano huo huku akivalia joho la kiongozi wa wake.
Hii ni licha ya kwamba, kiitifaki, kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua, ambaye alikuwa mgombea-mwenza wa Bw Odinga katika uchaguzi mkuu wa 2022 ndiye anayepaswa kushikilia taji hilo endapo kiongozi huyo wa ODM hatakuwepo.
Ndani ya ODM, duru zinasema kuwa vuta nikuvute ya chini kwa chini imeanza kushuhudiwa kati ya manaibu wa Bw Odinga, Wycliffe Oparanya na Ali Hassan Joho kila mmoja akitaka kumrithi kigogo huyo wa siasa za upinzani.
Hii ni licha ya Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna kukana kuwepo kwa mng’ang’anio wa kiti hicho akifafanua kuwa wadhifa wa kiongozi wa chama hakijatangazwa kuwa wazi.
Katika eneo la Nyanza, familia ya Odinga imeanza kujadili suala hilo huku majina ya wanasiasa yakitajwa.
Ijumaa wiki jana, mkewe Raila, Mama Ida Odinga alimpendekeza mwenyekiti wa ODM John Mbadi kuwa kigogo wa siasa za Nyanza baada ya mumewe kustaafu.
Isitoshe, mnamo Oktoba 8 mwaka jana kaka yake Raila, Dkt Oburu Oginga alimpigia upatu kiongozi wa wachache katika Bunge la Kitaifa James Opiyo Wandayi kuwa kigogo wa siasa eneo hilo.
Aliorodhesha sifa kadhaa za uongozi za mbunge huyo wa Ugunja alizosema zinamweka katika nafasi bora ya kuongoza jamii ya Waluo kisiasa “baaada ya Raila kustaafu”.
Lakini kwa mtazamo wangu yeyote ambaye anapania kumrithi Bw Odinga katika Azimio la Umoja-One Kenya, ODM na ngome yake ya Luo Nyanza anapaswa kudhihirisha siasa za ujasiri na kuwa mtetezi wa masilahi ya raia wa kawaida.
Sifa hizi mbili ndizo zimemwezesha Bw Odinga kujijengea himaya ya ufuasi sio tu katika ngome yake ya Nyanza bali katika maeneo mengine mengi ya nchi.
Kwa mfano katika muungano wa Azimio, wafuasi wake na Wakenya kwa jumla watamchukulia Bw Musyoka kuwa kiongozi wake ikiwa ataendeleza falsafa ya Bw Odinga ya kuikosoa serikali kila mara, hasa kuhusiana na masuala yanayolinda masilahi ya raia.
Hapa ninarejelea masuala kama vile nyongeza za ushuru, sakata za ufisadi serikalini na kupitishwa kwa miswada yenye mapendekezo yanayoendeleza utawala mbaya.
Mfano wa miswada hiyo ni ule unaolenga kumpa Rais William Ruto mamlaka ya kumteua mshauri wa Masuala ya Usalama.
Bw Musyoka anaweza kufanya hivyo kwa kuitisha mikutano kadhaa ya hadhara hasa jijini Nairobi kujadili masuala kama hayo.
Vivyo hivyo, Oparanya, Joho, Mbadi na Wandayi ambao wanapania kuvalia viatu vya Rais katika ODM na Nyanza mtawalia, wanafaa kudhihirisha sifa za kuwa watetezi wa raia.