MAONI: Bila mchujo, ODM isahau ushindi Kasipul na Ugunja
IWAPO chama cha ODM hakitaandaa mchujo kabla ya chaguzi ndogo za Kasipul na Ugunja, basi raia wawachague wagombeaji ambao wanaona watawatumikia vizuri.
Chaguzi hizi mbili ni kati ya zile zinazofuatiliwa kwa karibu sana.
Aliyekuwa mbunge wa Kasipul Charles Ong’ondo Were aliaga mnamo Aprili baada ya kupigwa risasi jijini Nairobi.
Kiti cha Ugunja nacho kilisalia wazi baada ya Opiyo Wandayi kuteuliwa Waziri wa Kawi mnamo Juni mwaka jana.
Hata hivyo, kuna mwenendo ambao unaendelea hasa Kasipul ambapo ODM inaonekana inalenga kumpendelea Boyd Were, mwanawe marehemu Ong’ondo Were.
Hata kabla ya babake kuzikwa, Boyd alionekana kuungwa mkono na baadhi ya viongozi wa ODM hasa wabunge Millie Odhiambo (Suba Kaskazini), Opondo Kaluma (Homa Bay Mjini) na Gavana Gladys Wanga.
Kwa sasa kuna madai kuwa maafisa wa kaunti wameingilia kampeni hizo na sasa wanampigia debe Boyd.
Ukweli ni kwamba ODM inaungwaji mkono Nyanza lakini enzi za kuidhinisha viongozi eti kwa sababu Raila Odinga amesema zilipitwa na wakati.
Katika eneobunge la Kasipul kuna wawaniaji wengi ambao wanataka kutumia tiketi ya ODM lakini jinsi ambavyo mambo yanaendelea huenda wakafungiwa nje na Boyd kupendelewa.
Kati ya wale ambao wangependa kutumia tiketi ya chama lakini wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa demokrasia chamani ni mfanyabiashara Philip Aroko.
Hii ndiyo maana wagombeaji kama Bw Moneybior wameamua kusaka kura kivyao badala ya kushughulikia tiketi ya ODM.
Kinachoshangaza ni kuwa uongozi wa ODM wenyewe umekaa kimya wala haujafafanua iwapo kutakuwa na mchujo kubaini mgombeaji maarufu.
Hii ni tabia ambayo chama hicho kimezoea katika kila uchaguzi hasa Nyanza ambapo huamka tu na kutangaza mwaniaji dakika za mwisho kuepuka kushiriki mchujo jinsi raia hutaka.
Mara hii raia wakae ange; wasiwachague viongozi tu eti kwa sababu wameidhinishwa na ODM, wahakikishe wameshiriki uteuzi.
Iwapo raia wa Kasipul watalazimishiwa Boyd Were na kuna mgombeaji mwingine maarufu wanayemtaka, basi wamchague.
Iwapo mchujo utaandaliwa na Boyd Were ashinde kwa haki pia wamchague.
Enzi za kuabudu ODM zimepitwa na wakati na Nyanza lazima izinduke kwa sababu viongozi wanachaguliwa kuwatumikia raia wala si tu kuonyesha uaminifu kwa Raila.
Kasipul ni eneobunge ambalo limekuwa na wabunge wachapakazi hivyo basi halistahili kupokezwa mwakilishi walo.
Oyugi Magwanga ambaye kwa sasa ni naibu gavana wa Homa Bay alikuwa kati ya wabunge waliokuwa na utendakazi wa kuridhisha alipohudumu kama mbunge wa Kasipul kati ya 2013-2017 na pia Kabondo Kasipul 2007-2013.
Marehemu Ong’ondo Were pia alikuwa mchapakazi na alikuwa akihudumu muhula wake wa pili.
Kwa hivyo, mshikilizi mpya lazima awe mchapakazi na kiongozi wa kusambaza miradi.
Ugunja, mkondo unafaa kuwa huo huo na iwapo ODM itakosea basi wafuate nyayo za majirani wao wa Ugenya ambao walimchagua David Ochieng’ kupitia tiketi ya MDG kutokana na utendakazi wake wa kuridhisha.
Wakati umefika ambapo wakazi wa Nyanza lazima wajiondoe kwenye minyororo ya kufungwa na ODM na waamue viongozi ambao watasaidia eneo hilo kupiga hatua kimaendeleo.