Maoni

MAONI: Fedha za raia zikitumika vizuri hawatasita kulipa ushuru zaidi

Na CHARLES WASONGA May 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

INASIKITISHA kuwa afisa wa hadhi ya Katibu katika Wizara ya Fedha Chris Kiptoo bado hajang’amua hisia za Wakenya kuhusu jinsi serikali inavyotumia pesa wanazolipa kama ushuru.

Akijibu maswali kuhusu Bajeti na Mswada wa Fedha wa 2025, Jumanne asubuhi katika kipindi cha “Fixing The Nation” kwenye runing ya NTV, Dkt Kiptoo alionekana kuwahimiza Wakenya wakubali kulipa viwango vya juu vya ushuru “endapo kuna mantiki ya kufanya hivyo.”

Kulingana na Katibu huyo, ni kupitia ulipaji ushuru wa juu ambapo taifa hili litajiondoa katika ‘utumwa’ wa kutegemea mikopo kufadhili mipango na miradi yake.

Lakini manahodha wa kipindi hicho, Eric Latiff, Janet Mbugua na Miriam Bishar, walimpohoji ubadhirifu wa pesa za umma na ufisadi unaendelea serikali, Dkt Kiptoo alikuwa mwepesi wa kuitetea serikali au kukwepa kutoa maelezo ya kuridhisha.

Kwa mfano, alitetea mpango wa serikali wa kutumia Sh2.5 bilioni kufadhili ukarabati wa Ikulu ya Nairobi na Ikulu zingine ndogo, hadi 2027 ilhali sekta muhimu kama elimu na afya zinakabiliwa na uhaba wa fedha.

Katika bajeti ijayo ya mwaka wa kifedha wa 2025/2026, kulingana na Dkt Kiptoo, Wizara yake imetenga Sh800 milioni kwa shughuli hizo.

Aidha, afisa huyo alichelea kuelezea mantiki ya Rais kuendelea kuajiri washauri katika afisi yake, wanaofyonza Sh1 bilioni kila mwaka, ilhali mwaka jana aliahidi kuwa idadi ya maafisa hao itapunguzwa kwa asilimia 50.

Kimsingi, Wakenya watakuwa radhi kulipa viwango vya juu vya ushuru ikiwa fedha hizo zitatumika kwa shughuli zinazowafaidi.

Ulipaji ushuru ni jukumu la mwananchi kwani ndio chanzo kikuu cha fedha zinazoendesha shughuli za serikali.

Lakini kinachowaudhi ni kwamba, wanapotozwa viwango vya juu vya ushuru, serikali inaelekeza fedha hizo katika shughuli zisizo na manufaa ya moja kwa moja kwao.

Pili, raia hukerwa hata zaidi kiasi kikubwa cha fedha wanazotoa kama ushuru zinaporwa katika sakata mbalimbali za ufisadi, wahusika wakuu wakiwa viongozi wandani wa wenye mamlaka nchini.

Kinaya ni kwamba, serikali imedinda kabisa kuzitengea asasi za kupambana na ufisadi fedha za kutosha za kuziweza kuziba mianya inayotumiwa na maafisa kuendeleza uovu huo au kuchunguza sakata hizo hadi kuhakikisha wahusika wanakamatwa na kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria.

Kwa mfano, katika mwaka ujao wa kifedha (2025/2026) Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imetengewa Sh3.2 bilioni pekee huku Afisa ya Mdhibiti wa Bajeti (CoB) ikitengewa Sh2.4 bilioni pekee.

[email protected]