Maoni

MAONI: Gachagua apambane na Ruto hapa nyumbani si huko Amerika

Na CECIL ODONGO August 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Naibu wa Rais Rigathi Gachagua anastahili kuwa mzalendo na kufahamu kuwa Kenya ni nchi huru wala haiko chini ya uongozi wa Amerika.

Wiki jana, Bw Gachagua alisema kuwa yuko tayari kufichua maovu ya utawala wa sasa kwa Amerika, akisema ana “mabomu” ya siri za serikali aliyoyapata alipokuwa akihudumu kama naibu wa rais kabla ya kung’olewa mamlakani mnamo Oktoba mwaka jana.

Kati ya “mabomu” aliyosema, ni jinsi ambavyo Rais Ruto anavyoshirikiana na kundi la wapiganaji wa RSF kuhakikisha serikali ya Sudan haina uthabiti wowote wa kisiasa na uongozi.

Aidha, alishutumu Rais Ruto kwa kushirikiana na magaidi na makundi ambayo yameharamishwa na Amerika.

Aidha, wakati wa ziara yake Amerika, Bw Gachagua amekuwa akipayuka katika kila mkutano, akisawiri Kenya vibaya na kusema kuna ukiukaji mkubwa wa haki za kibinadamu unaendelea nchini.

Mwanzo, ziara ya Bw Gachagua Amerika ilidhaniwa kuwa ilikuwa ya kukutana na kuuza sera zake kwa Wakenya huko, lakini imegeuka kuwa ya kukejeli na kuipaka tope nchi machoni pa ulimwengu.

Hata Kiongozi wa ODM, Raila Odinga, amekuwa na tofauti kali za kisiasa na tawala zilizopita, lakini hakuna siku ambayo alienda nchi ya nje na kuanza kuzungumzia Kenya vibaya.

Amerika imewahi, mara si moja, kukashifiwa kwa kuingilia uchaguzi wa Kenya, lakini Bw Gachagua asifikirie kuwa sasa wataokoa jahazi lake la kisiasa linaloendelea kuzama.

Bw Gachagua aliondolewa madarakani kwa sababu ya ukabila, ambapo alikuwa akijali tu jamii yake kutoka Ukanda wa Mlima Kenya. Sasa ndiye huru, yuko kiguu na njia, akihuburi mabaya ya nchi na kutaka Amerika iingilie uongozi wa nchi.

Aliyekuwa naibu rais lau angemakinikia kujivumisha hapa nchini ili kujiongezea uungwaji mkono, badala ya kukesha akizungumzia mambo ambayo anajua hayataweza kumwongezea umaarufu wowote kisiasa.

Amerika haipigi kura Kenya, kwa hivyo hata Bw Gachagua akikesha huko na kusawiri nchi kama inayoshirikiana na magaidi, kura zake hazitaongezeka.

Ni vyema zaidi hata kuwa amemulikwa na baadhi ya Wakenya wanaoishi Amerika kama mwanasiasa mwenye ukabila, aliyejikita katika kuendeleza maslahi yake ya kibinafsi.

Swali ni je, Amerika ikiingilia kati na kuchunguza kisha kuiwekea vikwazo, itamnufaisha nini? Bw Gachagua anastahili kuwa mtu wa mwisho kuzungumza kuhusu masuala ya haki za kibinadamu.

Baada ya uchaguzi mkuu wa 2022 na maandamano ya upinzani mnamo 2023, Bw Gachagua alinukuliwa akisema waandamanaji wasiwatarajie polisi wawabusu wanapojitupa barabarani.

Wakati huo, alilewa mamlaka na aliona dhuluma kama kawaida, ilhali hata Amerika yenyewe ilitoa wito wa amani nchini.

Mbona wakati alikuwa serikalini na waandamanaji walikuwa wakiuawa hakuongea ama kuitaka Amerika iingilie kati?

Kenya imehimili mawimbi makali ya kisiasa, na iwapo utawala wa sasa umeamua kuegemea mrengo wa China, basi hamna tatizo – ni uamuzi wao.

Hii dhana ya Bw Gachagua kusawiri Amerika kama inayostahili kuabudiwa na Kenya haifai kabisa, na ni mtazamo wa mtu asiyeona mbali.

Bw Gachagua akumbuke kuwa hata akijinadi kwa Amerika, nchi hiyo si malaika na ina viwango vya juu vya umaskini hata kuliko baadhi ya maeneo nchini.

Sasa kama yuko upinzani na ndiye huyo anajipendekeza kwa Amerika, si ikitokea akafanikiwa kuongoza nchi siku moja atakuwa kibaraka cha Amerika?