Maoni

MAONI: Gen Z wana haki ya kudai utawala bora

Na DOUGLAS MUTUA May 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HIVI maafa yakitokea nchini Kenya, ni sawa kwetu Wakenya kujiliwaza kwa kusema kuwa haidhuru kwa maana maafa yanatokea katika mataifa mengine pia?

Ni sawa kukubali kwamba kufa kwa wengi harusi, yaani tujiweke katika mazingira ya kufa kwa kuwa wengine wanakufa? Huo ni mtizamo wa aina gani katika karne hii?

Wakati mmoja Rais wa Amerika, Donald Trump, labda baada ya kuchoshwa na lawama kwamba ni mbaguzi wa rangi, alijaribu kujitetea: “Mimi si mbaguzi wa rangi pekee, kuna wengine wabaya zaidi.”

Tamko hilo, kutoka kinywani mwa mtu anayepaswa kuwa na mamlaka ya juu zaidi duniani, linaudhi na kuchekesha vilevile. Mtuhumiwa hakatai ana shida, ila anasema yake si kubwa kama ya watu wengine. Kimsingi, anakiri makosa yake.

Maneno yake hayo yalichanganuliwa kwa mapana na marefu, ikatokea kwamba hakika mwenyewe hakujua kwamba alikiri makosa, labda kutokana na kukolea kwa chuki yake dhidi ya watu weusi.

Mwanahabari fulani wa kimataifa aliangua kicheko na kufananisha mtizamo huo na mtu anayekiri kuwa ana changamoto ya unene, ambayo ni hatari kwa afya, ila anajiliwaza kwa kusema kuwa hawi mtu pekee aliye na tatizo hilo.

Mtizamo huo unaashiria kuwa aliye na unene wa kutishia afya yake hajali sana ikiwa unene wenyewe utakuja kumuua, eti kwa sababu watu wengine wanene watauawa nao pia. Hizo ni fikra finyu, za kipumbavu sana.

Juzi nimewatazama wabunge wetu wakichachamaa na kulikashifu shirika la habari la British Broadcasting Corporation (BBC) kwa kuandaa makala ya ukumbusho wa maandamano yaliyotokea nchini Kenya mwaka jana yakiongozwa na kizazi kichanga – Gen Z.

Mbunge wa Mandera Kaskazini, Meja Bashir Abdullahi, alihoji kwamba BBC iliionea Kenya kwa sababu kumekuwa na maafa kwingineko, lakini shirika hilo halikuandaa makala kama hiyo.

Aliuliza kwa nini BBC haikuandaa makala maalum kuhusu uvamizi wa majengo ya bunge la Amerika uliofanywa na wafuasi wa Rais Trump mnamo tarehe 20, mwezi Januari, mwaka 2020.

Alilalamika kwamba hata jijini London, Uingereza, kumewahi kuwa na machafuko na wala BBC haikuyaangazia kama ilivyofanya kuhusu Kenya.

Alitoa pia mfano wa kile alichoita mauaji ya halaiki dhidi ya wanawake na watoto yaliyotokea katika Ukanda wa Gaza, Palestina, hivi majuzi na shirika hilo halikusema chochote.

Mbunge huyo alitaka tuamini kwamba ametazama makala zote za BBC, na tuamini kwamba Kenya inaonewa. Hajali ukweli kwamba vijana zaidi ya 60 waliuawa wakati wa maandamano hayo, na bado mauaji hayo hayajachunguzwa na kutafutiwa suluhu.

Mbunge wa Dagoretti Kaskazini, Bw John Kiarie, alifoka mambo mengi tu yasiyo na maana, ila aliniudhi alipodai eti mwenyewe alikuwa mwanahabari, na anajua hakuna habari isiyo na baba au mama.

Kauli hiyo ina maana kwamba habari zote unazosoma au kusikia kwenye vyombo vya habari, ikiwemo makala yangu hii, huwa zimefadhiliwa na watu fulani.

Nina tatizo na kauli hiyo kwa kuwa nimeifanya kazi hii kwa miaka 26, na sijawahi kusikia wala kuona gazeti ambalo linajazwa kwa habari za kufadhiliwa.

Habari si matangazo ya biashara.

Kabla ya mtu kudai kuwa hata naye ni mwanahabari, na kuinyooshea kidole cha lawama tasnia nzima ya uanahabari, akumbuke kuwa kamwe hawi mwanahabari bora duniani. Pia, hii ni taaluma inayosifika kwa kufichua manyanyaso ya nduli dhidi ya wanyonge.

Nakubaliana na mtu pekee aliyeonekana kuelewa mambo, au kutojitia hamnazo kuhusu hali iliyo nchini wakati huu, Mbunge wa Suba Kaskazini, Bi Millie Odhiambo.

Aliwahimiza wabunge waache kulalamika tu na kujipendekeza kwa utawala wa sasa wa Kenya, wajiulize kwa nini kizazi cha Gen Z kimejawa na hasira, washughulikie mambo yanayokikera, lau sivyo kilipuke tena! Je, kuna ukweli mwingine unaotaka kusikia isipokuwa huo?

Wanaodhani kwamba vijana wanapaswa kunyamazishwa au kufyekwa kama nyasi kwa sababu ya umri wao wakumbuke kwamba Kenya ni nchi yao pia, na wana haki zote za kudai utawala bora. Hilo, bila tafadhali ya mtu.

[email protected]