Maoni

Ghasia zinazozingira hafla za Gachagua zinaaibisha serikali

Na CECIL ODONGO January 26th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

GHASIA ambazo zimekuwa zikishuhudiwa katika mawanda ya kisiasa zinavunja moyo na kuzua wasiwasi kuhusu usalama wa nchi kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

Wikendi, ghasia zilizuka katika Kanisa la Witima, eneobunge la Othaya ambako aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua alikuwa amehudhuria ibada ya kanisa.

Picha zilienea mitandaoni zikionyesha jinsi ambavyo wanawake na watoto wadogo walikuwa wamefunikwa na moshi wa vitoza machozi wakitorokea usalama wao.

Aidha, picha nyingine zilionyesha jinsi Bw Gachagua na viongozi wengine walivyokuwa wakitorokea usalama wao kwa kutumia vijia vidogo kuhepa magenge.

Kumezuka gumzo iwapo ni mrengo wa Bw Gachagua unajiandalia na kujipangia ghasia hizi kisha kulaumu serikali au vinginevyo.

Shaka hii inaibuliwa na matamshi ya Bw Gachagua mwenyewe kuwa Mbunge wa Juja George Koimburi alijiteka nyara kuzuia kufika kortini mwaka jana.

Bw Gachagua wakati wa ‘masaibu’ ya Bw Koimburi alikuwa amedai kwamba mbunge huyo aliteswa na kikosi cha maafisa wa usalama ‘wauaji’.

Alidai hata mbunge huyo alilazimishwa kupumua kemikali hatari ambayo iliathiri sauti yake wala hangeweza kuzungumza, kwa hivyo alikuwa akizungumza kupitia maandishi.

Bw Gachagua wakati huo alidai kuwa Rais William Ruto, Waziri wa Usalama Kipchumba Murkomen na Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Eliud Lagat walikuwa na nia ya kuwaandama wanasiasa wanaoegemea mrengo wake na pia kumzidishia masaibu kwa kumlenga.

Kukiri kwamba Bw Koimburi alijiteka nyara ilhali miezi michache tu iliyopita alitoa madai mazito kuwa serikali ilijihusisha na yaliyomfika mbunge huyo kunafanya iwe vigumu kumwamini Bw Gachagua kuhusu fujo zinazokumba mikutano yake.

Ingawa hivyo, hoja si nani anajisakia umaarufu au huruma kutokana na visa hivi ila ni taswira inayojitokeza katika jamii.

Mikutano ya Bw Gachagua ukanda wa Mlima Kenya imekuwa ikizingirwa na ghasia. Kabla ya tukio la wikendi, vijana waliokuwa wamebeba bakora wakidaiwa kusindikizwa na maafisa wa usalama, walitishia kusambaratisha mkutano wake mjini Nyeri.

Pia katika mkutano huo wiki mbili zilizopita, Bw Gachagua alisema kuwa serikali inamwaandama kwa kutumia wahuni katika ngome yake ya kisiasa.

Serikali inastahili kuchunguza ghasia zinazoandama mikutano ya Bw Gachagua eneo la Mlima Kenya kufahamu kweli ikizingatiwa sasa imefikia hali hatari.

Ni dhahiri kwamba uhasama kati ya Bw Gachagua na viongozi wa eneo la Mlima Kenya wanaoegemea mrengo wa serikali ndio unaleta fujo hizi za kuaibisha.

Aliyekuwa naibu rais amekuwa akiwataja baadhi ya wabunge kuwa wanahusika na kuratibu fujo dhidi yake.

Madai haya yachunguzwe na ukweli ubainike kwa sababu wanaotumiwa kutibua mikutano ya Bw Gachagua Mlima Kenya ni vijana na maafisa wa usalama.

Pia iwapo sasa wanasiasa wanatifuana na uchaguzi umesalia miezi 20 hivi, itakuwa aje kura za 2027 zikikaribia?

Bw Gachagua mwenyewe amedai kuwa uvamizi dhidi yake una mipaka kauli ambayo inaweza kufasiriwa kuwa naye huenda pamoja na watu wake wakalazimika kujilinda.

Hali ikifikia hivi, wanasiasa watakuwa wakiwatumia vijana kupambana na kando na uharibifu, mauaji yanaweza kutokea pia.

Katika haya yote, vijana nao wajihadhari hata kama uchumi ni mgumu kwa sababu hakuna tija kwa kumpigania mwanasiasa ambaye kesho pengine ataungana na huyo adui wake mnayemkabili kwa sasa.