Maoni

MAONI: Haikubaliki Kenya kupuuza sheria za kimataifa kwa kuteka nyara wakimbizi wa kisiasa

Na DOUGLAS MUTUA October 29th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

KENYA si taifa salama kwa wakimbizi wa kisiasa, kisa na maana haliheshimu sheria za kimataifa zinazowalinda.

Hii ina maana kwamba jumla ya wakimbizi 780,000 wanaojificha nchini wanaweza kukamatwa na kupigwa bei iwapo wanahitajika walikotoroka.

Yeyote aliyejificha Kenya anapaswa kufanya kila awezalo ili kukimbilia nchi nyingine kabla hajakamatwa na kukabidhiwa watesi wake aliokusudia kuwa mbali nao alipotoroka.

Asipofanya hivyo, basi ajue anakabiliwa na hatari ya kurejeshwa kwao, awakabili ana kwa ana viongozi wa kiimla ambao alikusudia kutofikiwa nao kwa vyovyote vile.

Kwa muda mrefu, wananchi wa mataifa ya Afrika wamekuwa wakilalamika kwamba wakikimbilia Kenya ili kuepuka manyanyaso ya kisiasa wanakamatwa kimya-kimya na kurejeshwa kwao bila hiari yao.

Kwa kiasi kikubwa, malalamiko hayo yametolewa na raia wa Ethiopia, Sudan Kusini, Uganda na hata Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na kadhalika.

Waethiopia hasa walianza kulalamika mara tu serikali ya awamu iliyopita ilipoingia mamlakani kwamba wakimbizi kutoka nchi yao wakifagiliwa mijini na hata kwenye kambi na kurejeshwa kwao ambako aghalabu wakiteswa na kuuawa.

Wapo wakimbizi wa kisiasa waliokamatwa nchini Kenya na kurejeshwa Sudan Kusini, wakakabidhiwa serikali na kutoweka wasipatikane tena mpaka leo, jambo ambalo limewafanya wengi ama kutoroka Kenya au kuiambaa kama jini au shetani.

Huo ni ukiukaji wa sheria za kimataifa na za Umoja wa Mataifa (UN) ambazo zinaziwajibisha nchi binafsi kuwahifadhi na kuwasaidia wakimbizi.

Unaposoma makala hii, Kenya inalaumiwa kwa kuwakamata wakimbizi wa kisiasa na kuwarejesha nchini Uturuki ambako wamekuwa wakitafutwa kwa miaka mingi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni, Dkt Korir Sing’oei, amekiri bila aibu kwamba Kenya iliombwa na Uturuki na ikakubali kuwakamata na kuwarudisha kwao Mustafa Genç, Öztürk Uzun, Alparslan Taşçı, na Hüseyin Yeşilsu. Walishukiwa kuwa na maoni tofauti na ya serikali ya dikteta Recep Tayyip Erdogan.

Ilikuwa vigumu kwangu kuamini kwamba Dkt Sing’oei, mwanasheria msomi, alikiri hadharani kuwa Kenya imevunja sheria za kimataifa.

Kibaya zaidi ni kisingizio alichotoa: “Tuliombwa na Uturuki tuwakamate raia wake hao na kuwarudisha kwao, nasi tukakubali baada ya kuhakikishiwa na serikali ya nchi hiyo kwamba itaheshimu haki zao.”

Kila mtu aliye na cheo cha Dkt Sing’oei anajua Uturuki ni mtuhumiwa mkuu wa ukiukaji wa haki za binadamu, hivyo kwake yeye kuamini ahadi hiyo ni kuonyesha kutojali kuhusu usalama wa watu hao wanaohitaji kulindwa na kutetetewa na kila mtu.

Kwa muda mrefu sasa, majasusi wa Uturuki wamekuwa wakiwafuata na kuwakamata au hata kuwaua watu wanaoikosoa serikali ya taifa hilo tajiri na lenye ushawishi mkubwa.

Mnamo mwezi Februari, mwaka 1999, Uturuki ilimtaja kuwa gaidi aliyekuwa mtetezi wa haki za jamii ya Wakurdi nchini humo, Abdullah Ocalan, kisha ikamfuata hadi Nairobi, ikamteka na kumrejesha nyumbani ambako aliteswa na kuhukumiwa kifo.

Baada ya nchi hiyo kuondoa hukumu ya kifo katika sheria zake, hukumu ya Ocalan ilibadilishwa na kuwa kifungo cha maisha gerezani, ambamo angalimo mpaka sasa kama mfungwa wa kisiasa.

Waliotekwa nyara jijini Nairobi hivi majuzi ni wakimbizi waliojiandikisha itakiwavyo, hivyo sheria za kimataifa zinawalinda kikamilifu. Kosa lao kuu ni kwamba walikuwa wafanyakazi wa shirika la kidini la Gülen lililojihusisha zaidi na elimu, na ambalo lilimikiliwa na msomi tajiri mno, Fethullah Gülen, mshirika wa zamani wa Rais Erdogan.

Bw Gülen, ambaye alifariki Jumapili iliyopita nchini Amerika alikoishi kama mkimbizi, amekuwa hasidi mkuu wa Rais Erdogan tangu watu walioshukiwa kuwa marafiki zake walipojaribu na kushindwa kupindua serikali ya Erdogan mnamo mwaka 2016.

Kila nchi ina matatizo yake ya ndani kwa ndani na inapaswa kutafuta mbinu za kuyasuluhisha kisheria bila kuitumia nchi nyingine kama uwanja wa kuyatatulia.

Jukumu la kwanza la serikali ya Kenya ni kulinda maslahi ya nchi, si kuwafurahisha viongozi wa kigeni hata ikiwa ni marafiki zetu.
Tunahitaji wawekezaji wa kigeni, si washirika katika kuvunja sheria za kimataifa.

[email protected]