Maoni

MAONI: Hatari za kujianika mitandaoni iwapo una ndoto ya kwenda Amerika

Na DOUGLAS MUTUA July 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 3

HIVI unanuia kwenda nje ya Kenya, kwa mfano Amerika, kusoma au kujaribu bahati ya kwenda huko kupitia ile bahati nasibu iitwayo ‘Green Card’?

Hebu tafakari ukitaka kuvuka mpaka na kuwatembelea jirani zetu, Tanzania, kisha wakutolee machapisho yako ukiwatukana mtandaoni kutokana na mambo yanayoendelea kwao. Utasazwa, uruhusiwe kuingia nchini humo, au utakamatwa na kufunguliwa mashtaka?

Je, unajua mzaha au matusi unayopakia mtandaoni yanaweza kukuponza sana unapojaribisha mambo fulani? Unafanya nini kuhakikisha kwamba hujinyimi fursa nyingi zinazopatikana katika dunia, hasa wakati huu ambapo imeunganishwa na mtandao na kuwa kama kijiji kimoja?

Na, je, unajua kuwa hata ikiwa unayaweka mambo yako wazi mtandaoni kimzaha, mtu mwingine anaweza kuyafasiri anavyotaka na huna uwezo wa kumkosoa, kuyakanusha wala kumshawishi aamini vinginevyo?

Tangu hapo kazi yako ni kuandika na kuchapisha au kupakia picha na video unakotaka, ila unaishia hapo. Kazi ya kuchambua na kuelewa mambo hayo ina mwenyewe na humjui, wala si ndugu yako. Huna nguvu; huna uwezo ziada ya hapo.

Juzi nimeingiwa na wasiwasi kuhusu mambo ambayo Wakenya wengi wanapakia kwenye mitandao ya kijamii – hasa X, Facebook, TikTok na kadhalika – baada ya Amerika kutangaza kwamba kila anayetaka kwenda kusoma huko sharti awape akaunti zake za mitandao ya kijamii.

Utawala mpya wa Rais Donald Trump umeamua kuwawinda na kuwazuia watu unaodhani hawaipendi nchi hiyo hata kabla hawajatia guu huko kwa kuwa umetambua kwamba wanafunzi wa kigeni wanapenda kushiriki maandamano na kuwashawishi wazawa wa Amerika.

Kimekuwa kibarua kigumu kwa utawala huo kuwafukuza baadhi ya wanafunzi wa kigeni walioonekana kwenye video wakishiriki maandamano kwa sababu wamekimbia mahakamani na kushtaki, majaji wakaamua hafukuzwi mtu! Kesi nyingine nyingi zinaendelea.

Na kwa kuwa mazoea yana taabu, utawala huo unaamini kwamba aliyeficha kitu moyoni dhidi ya Amerika atakuwa amewahi kukiandika mtandaoni angaa mara moja tu.

Wakifungua akaunti zako kisha wapate dalili kwamba hupendi chochote kuhusu Amerika, wanakunyima kibali cha kuingia kwao na hakuna hatua kitu chochote unachoweza kuwafanyia ila kuwanunia.

Bila shaka si kila Mkenya anayetaka kwenda kusoma Amerika, wengi wanataka kufika huko ili wafanye kazi na kuunda pesa za haraka kisha warejee nchini Kenya kufurahia maisha na uhuru wa walikozaliwa.

Wapo pia wasiotaka hata kusikia hiyo hadithi ya kuhamia Amerika, lakini wanatamani kutoka nje ya Kenya ili wakajaribishe bahati ya maisha kwingineko kwa kuwa labda Kenya hakuwakai, maisha yamekuwa magumu, au wanatamani tu kubadilisha mazingira.

Tatizo ninaloona kuhusu uamuzi huo wa Amerika ni kwamba mara nyingi mataifa ya dunia, kwa ajili ya kujilindia maslahi, huiga mambo ambayo yanafanywa na taifa hilo tajiri na lenye ushawishi mkubwa zaidi.

Unaweza kusikia mataifa yote ya Uropa yameanzisha sera kama hiyo, ghafla iwe vigumu kwa wanoko wa mtandaoni kwenda popote, na labda wamekuwa wakichapisha huko mambo ya kutania na kujifurahisha tu.

Uamuzi huo wa Amerika ya Trump unaweza kuonekana kama uko mbali sana na Mkenya wa kawaida, lakini kumbuka bahati nasibu ya ‘Green Card’ hufanyika mwanzoni mwa Mwezi wa Kumi kila mwaka, tena yeyote, hata mfugaji mbuzi aliye kijijini, anaweza kujaribu bahati yake.

Hali inaweza kuwaje ukibahatika katika kamari hiyo, kisha unapofika kwenye ubalozi wa Amerika kwa ajili ya usaili wa visa ya kusafiria uambiwe huwezi kuruhusiwa kuingia nchini humo kisa na maana vitu vya kipuuzi ulivyofanya mtandaoni? Utawahi kujisamehe? Utaambia watu nini?

Labda hili lilikupita, lakini mwanahabari Mkenya, Idris Muktar Ibrahim, alifutwa kazi na shirika la CNN miaka miwili iliyopita kwa sababu ya mambo aliyochapisha kwenye ‘Twitter’ tangu akiwa na umri wa miaka 15!

Mwanahabari huyo aliyezaliwa na kukulia mtaani Korogocho, Nairobi, alifutwa kazi kwa kile kilichodaiwa kuwa chuki yake dhidi ya Wayahudi, kutokana na mambo ya kimzaha aliyochapisha mtandaoni akiwa mtoto bila kujua siku moja atainuka na kuvuma kimataifa.

Wakati huu ambapo duniani kumejaa machafuko, hasa vita vya Israel na Iran, nakutafadhalisha uwe makini sana unapoweka vitu mtandaoni kwa kuwa vinasomwa kote-kote, nao mtandao hausahau.

Mtu akitaka kujua mitazamo yako kuhusu mambo fulani, ataingia tu kwenye mtandao na kupata kila kitu ulichoandika. Na itakuwa vigumu kujitetea ikiwa yatakuwepo ya kukuweka katika hali tatanishi. Wakati mwingine unaandika mambo na kusahau, lakini yanakuandama daima.

Wala asikwambie mtu kwamba una uhuru wa kujieleza, sheria zinakuruhusu kusema yoyote unayotaka, vyovyote unavyotaka. Anayekwambia hivyo anakuhadaa mchana kweupe. Nyakati huwadia ukakosa kwa kudai haki zako hizo.

Hayo ya haki za kila aina ni maneno mazuri yakitamkwa, hasa katika muktadha wa siasa, lakini ukifanya kitu kinachoonekana kuhatarisha usalama wa nchi yoyote ile, hata Kenya, utakwenda kusemea mbele, mbali na mashabiki wako ambao kila wakati wakikuchochea mtandaoni.

Wasia wangu? Usisahau akili nyumbani unapoingia mtandaoni. Furahia maisha, tamba unavyotaka, pata kuwapendeza na kuwaburudisha wengi, lakini daima kumbuka mtandaoni kuna watu wanaokusanya ushahidi kuhusu mambo unayoyafanya. Usijipalie makaa bure.

mutua_muema@yahoo.com