Maoni

MAONI: Heri tuwavumilie viongozi waliopo hadi uchaguzi ujao kwa manufaa ya ustawi

Na KINYUA KING'ORI May 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

HUWA nashangaa, mbona Wakenya wameonyesha ishara za mapema za kuchoshwa na viongozi wao kiasi cha kuwachukia?

Kenya ni taifa la kushangaza ambalo raia wanaongozwa na viongozi waliowachukia na kukosa imani nao.

Wananchi watakosaje kukosa imani na viongozi wao ikiwa wanachama wa UDA na ODM hawawezi kuaminiana kutekeleza mkataba wa makubaliano waliotia saini Machi 7, 2025, licha ya kushirikiana katika serikali jumuishi?

Je, ikiwa vinara wakuu katika mkataba huo; Rais Ruto na Raila, hawana uhusiano mwema wanatarajia wafuasi wao wakumbatiane kwa upendo?

Itakuwa vigumu taifa kuendelea kufanikisha maendeleo, uchumi, usalama na umoja pasipo kwanza viongozi na wananchi kupalilia uhusiano bora, kujenga ushirikiano bora na kuhakikisha masuala muhimu yanayoibua ukosefu wa imani yameshughulikiwa haraka.

Wanachi wanafaa kuwaheshimu viongozi waliowachagua hata kama hawajatekeleza ahadi zao hadi wamalize kipindi chao cha miaka mitano kwa mujibu wa katiba.

Ni utukutu kwa raia kuvuruga mikutano ya kisiasa ya viongozi, kuwatupia mawe au viatu na kutatiza michezo ya soka nchini kwa kuharibu viwanja na kusababishia taifa hasara kwa sababu ya miegemeo ya kisiasa kama ilivyoshudiwa eneo la Gusii majuzi.

Hasira ya raia huenda inachochewa na tabia ya wanasiasa kuwapuuza na kutoa matamshi yanayowakera.

Ukosefu wa uhusiano mwema na ushirikishwaji wa umma ulichangia Mswada wa Fedha 2024 kutupwa na kukosesha serikali fedha kutimiza ahadi zake.

Raia wanafaa kujua viongozi waliowachagua si malaika kwa sababu wengine wanatumia mamlaka yao visivyo na kufuja fedha za umma.