MAONI: Hivi ndivyo Rais Ruto anavyopaswa kuongoza nchi
KATIKA mazingira ya siasa kali ambapo watu wanatishiana, haidhuru nikijaribisha uungwana, nijitie udarai wa kumshauri kiongozi wa nchi jinsi ya kuwa rais bora na wa kupendeza tena.
Nimesalitika kujaribisha uungwana baada ya kumwona Rais William Ruto na wafuasi wake sugu waliomchagua wakisisitiza mitandaoni kwamba Uchaguzi Mkuu ujao utafanyika mnamo mwaka 2027.
Kwa hivyo? Eti yeyote anayeota kwamba anaweza kumshuritisha Dkt Ruto kung’atuka kabla ya wakati huo anatwanga maji kwa kinu akitarajia yampe unga.
Siamini umefika wakati wa kukumbushwa kwamba tuzitayarishe kura zetu, ila tusubiri hadi mwaka 2027.
Afua ni mbili: Ama mihemko na fujo za kizazi kipya, almaarufu Gen Z, imemwogofya mno Dkt Ruto na wafuasi wake, au wamezidi kwa jeuri kiasi kwamba hawajali kelele za vyura wanaojaribu kumzuia ng’ombe kunywa maji.
Niruhusu niamini kwamba Rais Ruto ameshtuliwa na matukio ya hivi majuzi ambapo Gen Z wametokea kutosikia la mwadhini wala la mteka maji msikitini. Hawasemezeki.
Walimshinikiza kuondoa Mswada wa Fedha wa 2024, sasa wanamwambia, tena kwa kufoka: “Anguka nao!” Kimsingi wanamshurutisha ang’atuke kutoka mamlakani, hawamtaki.
Sioni ajabu kwa watu wasiompenda kiongozi wao kumwambia ajiengue kabla ya muhula wake wa kutawala kufikia kikomo; tumemsikia kinara wa Upinzani, Bw Raila Odinga, na wenzake wakisema hivyo tangu mwaka 1992.
Hata hivyo, Raila na wenzake hawajawahi kuyatia moto majengo ya Bunge kama walivyofanya vijana wa Gen Z.
Tuliwazoea Raila na wenzake wakitishia kuongoza maandamano hadi Ikulu, kwenda kumng’oa mwenyeji wake, lakini tulijua ni porojo tu.
Hebu tumbua macho vizuri uone maajabu yanayofanywa na Gen Z. Wakisema watafanya kitu, wanakifanya. Wakisema maandamano yao yanaaza saa sita adhuhuri, yanaanza wakati huo. Na wakiahidi kutia moto majengo ya watu, unashtukia moshi ukifuka kutoka humo!
Wasiloweza kufanya kufikia sasa ni kuitwaa na kuikalia Ikulu, lakini ni siri iliyo wazi kwamba wana nia ya kufanya hivyo, tena wanaitangaza nia hiyo mtandaoni.
Wakati ambapo Mswada wa Fedha wa 2024 uliondolewa na maandamano yakaendelea, nilijiuliza yana umuhimu gani, hasa kwa kuwa kilichowakera kilifutiliwa mbali, ila baadaye niliwaelewa.
Ukitaka kuwaelewa Gen Z, unahitaji tu kujua kwamba Mswada wa Fedha ni kero iliyowasababisha kulipuka, ila haiwi kero ya pekee nchini Kenya.
Gen Z wamekerwa na ufisadi nchini Kenya. Wamekerwa na mazoea ya serikali kuwatumikia Wakenya kwa kiburi kana kwamba inawafanyia hisani.
Wamekerwa na baadhi ya nyuso ambazo zinaonekana kwenye baraza la mawaziri. Hawataki kuwaona watu waliokabiliwa na sakata za kila aina kisha mashtaka yakaondolewa ili wawe mawaziri.
Wanajiuliza iwapo Kenya imepungukiwa na watu wenye maadili kiasi kwamba Rais Ruto analazimika kuwateua mawaziri Bw Mithika Linturi, Bi Aisha Jumwa na wengineo.
Je, hao ndio vielelezo bora nchini? Kabisa hatuna wengine wenye sifa nafuu?
Ningekuwa Rais Ruto, ningecheza kamari kama Rais Kagame wa Rwanda, niwe sehemu ya, na wala si kizingiti dhidi ya, mabadiliko yanayonukia nchini.
Ningewafuta kazi mawaziri wote usiku mmoja, kisha siku inayofuata niwateue wengine wasiowapa Wakenya kinyaa!
Baraza langu jipya lingekuwa na mawaziri 12 pekee, wasio na wasaidizi, na wote wangekuwa na umri wa chini ya miaka 35.
Wote wangekuwa wataalamu wasiojulikana kitaifa, sikwambii kimataifa, na jukumu lao lingekuwa kuwahudumia Wakenya kwa uadilifu wa hali ya juu, lau sivyo wafungwe jela kisheria!
Wazee waliozoea kushikilia nyadhifa za uwaziri na nyinginezo kubwa serikalini ningewatafutia makosa ili ama niwanyamazishe au niwafungulie mashtaka kikweli, walioibia umma warejeshe walichoiba, lau sivyo waozee jela!
Huku moto wa mabadiliko ukiendelea kuwaka, ningeishawishi Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) iwasajili upya wapigakura, shughuli yenyewe iongozwe na Gen Z ili wahamasishane kujiandikisha, nimthubutishe yeyote kunipinga mwaka 2027.