Maoni

MAONI: Hivi ndivyo Ruto anafumua Upinzani kimya kimya kabla ya 2027

Na BENSON MATHEKA September 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

DALILI zimeanza kuonekana wazi kuwa Rais William Ruto anatekeleza mkakati wa kisiasa uliosukwa kwa ustadi mkubwa wa kuvuruga upinzani taratibu kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027.

Mbinu anazotumia si za mabavu moja kwa moja, bali ni hatua zinazoonekana kama za kiungwana, lakini kimsingi zinapunguza makali ya upinzani na kuufanya usieleweke na umma.

Kuwazuia wanasiasa wa upinzani kuandaa mikutano ya hadhara katika maeneo mbalimbali, hususan ngome za upinzani au zile zinazoonekana kugawanyika, ni mkakati wa kuhakikisha hakuna nafasi yao kuonekana wakivutia umati au kuungwa mkono na Wakenya wengi.

Pili, hatua ya kuanza kuwavuta viongozi wa mashirika ya kijamii na wanaharakati kwa kuwateua katika majopo na nyadhifa serikalini ni ishara nyingine ya kuufumua upinzani kimya kimya.

Hawa ni watu walio na sauti huru ya kuikosoa serikali, lakini sasa wanazimwa kwa kupewa vyeo — ujanja unaoonekana kama heshima kwa juhudi zao, lakini kiuhalisia ni mbinu ya kuwasilisha serikali kama inayokumbatia ushauri, huku ikiziba njia ya ukosoaji wa wazi.

Mbali na hayo, serikali imeanza mchakato wa kufidia waathiriwa wa maandamano yaliyoshuhudiwa mwaka jana.

Hili ni jambo jema kwa misingi ya haki za binadamu, lakini pia linaonekana kama mkakati wa kisiasa wa kutuliza hisia za hasira dhidi ya serikali.

Hii ni hatua ya kuondoa athari na makovu ya maandamano ya upinzani kwa njia ya maridhiano ya kifedha.

Zaidi ya yote, Rais Ruto ameendeleza kampeni kupitia mikutano ya mashinani, ambapo hutangaza uwezeshaji wa mamilioni ya pesa kupitia makundi ya vijana, wanawake na biashara ndogo ndogo.

Huku akijenga taswira ya kiongozi anayeguswa na changamoto za mwananchi wa kawaida, Ruto pia anapunguza ushawishi wa upinzani ambao mara nyingi hutumia majukwaa hayo hayo kudai serikali haifanyi lolote mashinani.

Kwa mtazamo wa haraka, yote haya yanaweza kuonekana kama uongozi unaojali na unaojitahidi kusuluhisha matatizo ya wananchi.

Lakini kwa jicho la kisiasa, hii ni hesabu makini ya kupunguza nguvu ya upinzani kujijenga.

Matokeo yake ni kwamba ifikapo 2027, huenda serikali ikakumbana na upinzani dhaifu, usio na mshikamano, usio na ajenda ya pamoja hali ambayo ni hatari kwa demokrasia.