Maoni

MAONI: Hizi hapa sababu ukuruba wa Ruto na Gideon utamaliza Murkomen kisiasa

Na CECIL ODONGO October 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

UKURUBA mpya wa kisiasa kati ya Rais William Ruto na aliyekuwa Seneta wa Baringo, Gideon Moi huenda ukawa mwanzo wa mwisho wa siasa za Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen.

Katika siasa za Bonde la Ufa, Bw Murkomen amekuwa mwandani wa Rais Ruto kiasi cha kulinganishwa na jinsi marehemu Waziri Nicholas Biwott alivyokuwa kwa Rais Daniel arap Moi au Chris Murungaru katika kipindi cha utawala wa Rais Mwai Kibaki.

Biwott ambaye alikuwa mbunge wa Keiyo Kusini alikuwa mwandani wa Moi kiasi kwamba ushawishi wake ulihisiwa kwenye teuzi mbalimbali wakati huo.

Naye Bw Murungaru alikuwa ameaminiwa sana na Kibaki mwanzoni mwa utawala wake.

Ni kati ya wanasiasa wanaodaiwa kuwa kikwazo katika kutekelezwa kwa muafaka ulioafikiwa kati ya wanasiasa wa LDP na NAK kuelekea uchaguzi wa 2002.

Bw Murkomen amekuwa akiaminiwa sana na Rais Ruto kiasi kwamba amekuwa akizungushwa kutoka wizara moja hadi nyingine na kukwezwa cheo, hilo likihusishwa na urafiki wake na Rais.

Chini ya miaka mitatu, Bw Murkomen ameshikilia wizara tatu za hadhi na ni kati ya wanasiasa ambao wanadaiwa wanaweza kumfikia Rais wakati wowote bila kuzuiliwa.

Mwanzo alikuwa katika wizara ya hadhi ya uchukuzi kisha akahamishwa hadi Wizara ya Michezo baada ya maandamanao ya Gen-Z.

Wakati ambapo Prof Kithure Kindiki alikwezwa hadhi hadi kuwa naibu wa rais, Bw Murkomen alihamishwa na kujaza Wizara ya Usalama wa Ndani, wadhifa ambao anaushikilia hadi sasa.

Kwa kipindi cha miaka mitatu sasa, Bw Murkomen amekuwa kiongozi wa hadhi zaidi kutoka Bonde la Ufa ambaye amekuwa sura ya utawala wa Rais Ruto.

Hata hivyo, iwapo ukuruba wa Gideon na Rais utaendelea, ushawishi wa Bw Murkomen utapungua na itabidi ameze mate machungu na kukubali kuwa nyuma ya vigogo hao wawili wakuu.

Mwanzo, siasa za urithi wa 2032 katika Bonde la Ufa zitamfaa sana Gideon, 61 iwapo Rais Ruto atafaulu kuwahi muhula wa pili.

Gideon tayari anatokea familia ya rais wa zamani na anaonekana kama kiongozi ambaye ana sura ya kitaifa kuliko Bw Murkomen ambaye anaanzia chini kama waziri.

Ni rahisi sana kwa Gideon kutumia ufalme wa marehemu babake Mzee Moi kutanua mawanda yake nchini.

Pili, hatua ya Gideon kumeza shubiri na kukubali kufanya kazi na Rais Ruto si jambo ambalo lilitokea kwa urahisi.

Ukanda wa Bonde la Ufa ungeshuhudiwa mgawanyiko zaidi iwapo Bw Gideon angewania kiti cha useneta wa Baringo na kumbwaga mwaniaji wa UDA.

Iwapo siasa zingechukua mwelekeo huo, Rais Ruto angeponzwa kwa sababu ingekuwa dhahiri kuna tatizo katika ngome yake wakati ambapo naye anakabiliwa na kibarua cha kusaka muhula wa pili baada ya maasi ya Gen-Z mwaka huu na mwaka jana.

Hii ndiyo maana iwapo kuna minofu ambayo itamegwa na rais basi lazima Gideon apokezwe wadhifa wa hadhi zaidi.

Pia Rais kwa kinywa chake mwenyewe alikiri kuwa yeye ni mwanafunzi wa kisiasa wa Mzee Moi na anataka kuonekana kutokuwa na uhasama na familia hiyo.