Maoni

MAONI: Ikiwa Raila atanufaika na wadhifa wowote serikalini, autumie kuleta mabadiliko

Na KINYUA KING'ORI March 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

TANGU kinara wa chama Cha ODM Raila Odinga aonyeshe dalili za wazi kushirikiana na hasimu wake kisiasa Rais Ruto, amekuwa akizunguka katika ngome zake kisiasa katika vikao vya kushauriana na wafuasi wake akitarajiwa kutangaza mwelekeo wake kuelekea uchaguzi ujao 2027.

Lakini kile Raila hataki kusema ni kwamba tangu akome kuendeleza upinzani mkali kuhakikisha serikali hii inatimiza wajibu wake, upinzani ulififia maana hata Kalonzo ameshindwa kufikia kiwango chake kama Kiongozi wa Upinzani kwa sasa.

Je, Raila sasa akijiunga na serikali atawezaje kudumisha umaarufu kisiasa na kubadilisha mbinu zake za ukosoaji kusuta serikali anayounga mkono inapofeli kuwajibikia ahadi zake bila kusaliti mshirika mwenza Rais Ruto?

Je, Raila ataambiaje wananchi ambao wanapitia matatizo tele wanapoenda hospitalini na kukosa matibabu licha ya kuchangia bima mpya ya afya ya SHA kuunga mkono serikali hii inayowafelisha?

Japo si hatua njema, sipingi Raila kushirikiana na Ruto lakini muhimu awe makini asiye kudhibitiwa kwa kutiwa kidanga cha mdomo na minofu serikalini na kuwa bubu na masito vijana wa Gen-Z wakidai wenzao waliouawa wakati wa maandamano kufidiwa.

Akifanya hivyo atakuwa msaliti kwa vijana wa taifa hili waliojitokeza kupinga sera kandamizi zinazowaathiri na kuwasababishia changamoto nyingi.

Ikiwa Raila atanufaika na wadhifa wowote serikalini autumie kuleta mabadiliko kuondolea raia mzigo mzito wa ushuru wa juu, kuboresha bima ya afya SHIF, kulinda upinzani, kukomesha ufisadi na visa vya utekaji nyara, kuhakikisha Tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) imeundwa haraka, kulinda uhuru wa vyombo vya habari na kuimarisha usalama na maendeleo kote nchini bila miegemeo ya kikabila au kisiasa.

La mno wafuasi wa ODM na Wakenya kwa jumla wajue watanufaika na nini Raila na Ruto wakishirikiana si kuwatumia kujinufaisha wao na wandani wao tu.