MAONI: Imebainika siasa za ‘ndio bwana mkubwa’ haziwezi kuisha kwa urahisi
KUNDI la siasa la Kenya Moja limejitokeza kwa nguvu nyingi na kusema lina ajenda ya kujenga muundo mpya wa siasa Kenya.
Ni wabunge wanaodhania siasa za “ndio bwana mkubwa” zimeisha. Hawataki kuwa chini ya vivuli vya viongozi wahafidhina wa vyama.
Caleb Amisi wa Saboti anadhania muungano wa Rais William Ruto na Raila Odinga ni masilahi yao tu kuendelea kukaa madarakani kwa namna tofauti.
Kiongozi wa uasi wa kundi hilo seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna amepinga kwa dhati jaribio la kumpa Rais Ruto muhula mwingine. Yeye anapiga injili ya wantam.
Gathoni Wa Muchomba naye ambaye alikuwa karibu na naibu Rais aliyefukuzwa kazi Rigathi Gachagua ameamua kuchukua mkondo wake wa kujisimamia.
Kundi hili halijaamua linayemtaka kuwa mpeperushaji bendera kipenga cha kura kitakapolia. Hata hivyo kuna mambo chanya ambayo limefanya yatawatia wasiwasi Rais Ruto na hata viongozi wa upinzani.
Kwanza, Babu Owino ametangaza kuwa atagombea ugavana wa Nairobi katika uchaguzi mkuu wa 2027. Babu amekuwa maarufu mno hata sehemu za Nyanza ambayo ni ngome ya Raila Odinga.
Edwin Sifuna ni mtu ambaye sasa watu wanataka kumsikiza. Muchomba anatembea na majira Kiambu na maeneo jirani.
Viongozi hawa wamepata sifa kubwa ya kukashifu mauaji ya kiholela ya vijana wanaokosoa utawala wa Rais Ruto.
Anthony Kibagendi naye ni mwanamikakati hodari wa kupanga mikutano na maandamano tangu akiwa kiongozi wa wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Maseno.
Suala nyeti hapa ni je, wataendelea hivi hadi mwisho? Je, Kibagendi atajiondoa katika kikosi kinachomsukuma Dkt Fred Matiang’i kuwa Rais wa sita?
Je, Sifuna akipokonywa wadhifa wake wa katibu mkuu wa ODM atakuwa na msingi imara wa kujisimamia?
Naye Gathoni wa Muchomba atatafuta ridhaa ya watu wa Githunguri nje ya chama cha DCP ambacho kina umaarufu mlimani?
Awali, kumekuwa na makundi kama haya lakini yakafifishwa ama kutokomezwa kabisa na mabwana watawala. Katika bunge la nane, kulikuwa na kundi la wabunge sita waasi wa KANU.
Walijumuisha Cyrus Jirongo wa Lugari, William Ruto wa Eldoret Kazini, Kipkalya Kones aliyebeba matumaini ya watu wa Bomet, John Sambu wa Mosop, Joseph Kimkung wa Mt Elgon na fungakazi Kipruto Arap Kirwa kutoka vilimani Cherengany.
Moi alifanyaje? Aliwafanya jirongo kuwa waziri, Ruto akawa waziri msaidizi sawa na Kirwa japo Kirwa aliendelea kuwa mpambanaji hadi mwisho.
Walitawanyika baadaye kila mtu akashika njia yake baada ya uchaguzi mkuu wa 2002.