Maoni

MAONI: Kalonzo ajue kwamba urais haupeanwi, unapiganiwa uchaguzini

Na BENSON MATHEKA July 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KIONGOZI wa chama cha Wiper Democratic Movement, Kalonzo Musyoka, ni mwanasiasa mwenye uzoefu wa muda mrefu katika siasa za Kenya.

Ametumikia taifa katika nafasi mbalimbali, ikiwemo kuwa Makamu wa Rais, Waziri, na mgombea mwenza katika uchaguzi kadhaa wa urais.

Kwa sasa ametangaza kuwa atagombea urais katika uchaguzi mkuu wa 2027 akionekana kutegemea viongozi wengine wa upinzani kumuunga mkono na kumpigia debe.

Hili ni kosa ambalo wandani na washauri wake wanamfanyia hujuma kwa kutomweleza wazi.

Ni muhimu Bw Musyoka aelewe kuwa kiti cha urais hakipeanwi kama zawadi ya kisiasa; kinapiganiwa kwa nguvu, mikakati, na uungwaji mkono wa wananchi.

Katika nyakati za hivi karibuni, Kalonzo ameonekana kusisitiza kuwa ni zamu yake kupewa nafasi ya kuwania urais kupitia makubaliano muungano wa kisiasa ambao anawania kusuka akiwa na viongozi kama Fred Matiangi, Rigathi Gachagua, Martha Karua na wengineo.

Ingawa siasa za miungano na maelewano ni sehemu ya demokrasia yetu, ni muhimu kutambua kuwa wananchi ndio waamuzi wa mwisho.

Siasa za sasa zinahitaji viongozi wanaojitokeza kuonyesha sio tu maono makubwa, uwezo wa kuongoza taifa na kushughulikia changamoto zinazowakabili Wakenya wa kawaida bali pia ujasiri usioyumba.

Wakenya hawakubali tena viongozi wanaotegemea huruma za kisiasa au kumbukumbu za makubaliano ya nyuma ya pazia.

Wanahitaji mtu mwenye dira, thabiti, na nguvu za kisiasa za kuzunguka nchi nzima akijenga uungwaji mkono kutoka kwa wananchi wenyewe.

Kama Kalonzo ananuia kuwa rais wa Kenya, basi ni wakati wake kuacha siasa baridi za kusubiri “kupokezwa” na badala yake ajitokeze hadharani, aeleze sera zake, awavutie wananchi, na aonyeshe kwamba anaweza kupambana na wengine kwa njia ya haki, wazi, na ya kidemokrasia.

Urais hauombwi — unapiganiwa. Na ni wananchi pekee ndio wenye mamlaka ya mwisho ya kumpa mtu kiti hicho.