MAONI: Kifo cha Jirongo kimeibua maswali tele kuliko majibu
ANGALIKUWA mtumishi wa umma, angalikuwa amestaafu na p engine kujishughulisha na mambo yake. Angalikuwa na nguvu za kuwashawishi Wakenya, angalikuwa Rais wao mnamo 2017.
Watu wa Kakamega walimyima fursa ya kuwa gavana wao katika uchaguzi mkuu wa 2022.
Wakazi wa eneo bunge la Lugari walimpa na kumnyima ridhaa ya kuwaongoza kwa nyakati tofauti.
Ni mheshimiwa marehemu Cyrus Khashalaga Jirongo. Alikuwa mbunge wangu mara mbili na tulimwita CJ. Sasa roho yake imepotea ghafla katika mazingira ya kutatanisha.
Pamoja na hayo, kiongozi huyo wa chama cha UDP amethibitisha msemo kuwa anapokufa mtu huwaachia mengi walio nyuma.
Moja ya mitihani aliowaachia Wakenya ni kutambua chanzo cha kifo chake.
Vyombo vya usalama vimo mbioni kutafuta taarifa za kuridhisha. Alikuwa mtetezi mkubwa wa jamii ya waluhya, koo yake ya Watiriki inalengwalengwa na michirizi ya machozi.
Mwanafunzi huyo wa zamani wa Mang’u ameenda mbele za haki.
Kifo chake kinachosadikiwa na “baadhi” kuwa kilitukia majogoo Jumamosi maeneo ya Naivasha kimebeba karai kubwa ya maswali.
Wameuliza watu alikuwa wapi na nani na akifanya nini kabla kukosa kusema tena.
Baadhi wamekiri walikutana naye kabla ya kuhama dunia. Mashuhuda wa ajali hiyo wamekuwa wachache mno na kutoa hoja kinzani.
Hapumui Jirongo aliyejigamba vijijini kuwa alikuwa na macho makubwa yaliyopendeza na wakati mwingine kuwatambua warembo kwa dharura.
Si maneno yangu alisema alipompoteza bintiye mwaka huu.
Nilimwona mara ya kwanza nikishaelewa dunia kiasi mwaka wa 1997. Alipita vijijini akawaletea kina mama kanga na sukari kwa wingi.
Wanaume walipewa hela kuwashawishi wampigie kura. Akawa mbunge wetu wa Lugari. Alikutana na yeyote na kusema na yeyote.
Afisi yake pale Loita House ilikuwa hifadhi kubwa ya watu kutoka Sinoko, Mawetatu, Kongoni, Mautuma na ha Lumakanda.
Inasemekana yeye na kundi lake la Youth for KANU 92 waliharibu uchumi wa nchi.
Aliandamwa pia na kashfa nyingi zikiwemo za ardhi. Akatengwa kama jini na jumuiya ya wanasiasa. Alipotangazwa mfilisi, watu wakasahau hisani yake alipokuwa hai.
Sasa amesafiri njia ya marahaba. Akiitwa haitiki, hatafanya chochote mwanapatholojia akiichunguza maiti yake.
Amekata roho na ujasiri moyo, kinywa chake kilikuwa nyumba ya ufasaha na ubongo wake ulikuwa miliki ya akili tendaji.
Sikujua za “ndani” sana kumhusu lakini nilitangamana naye kwa faragha na hadharani. Waziri huyo wa zamani alikuwa mtu safi wa gumzo mjini na kijijini.
Paul Nabiswa ni mhariri, NTV