Maoni

MAONI: Kiswahili kitumike katika mchakato wa uteuzi wa majaji unaoendelea

Na AKUNGAH O’NYANGERI January 19th, 2026 Kusoma ni dakika: 1

LUGHA si chombo cha mawasiliano tu bali ni mhimili wa haki. Haki ya kusikilizwa na kueleweka inategemea, kwa kiasi kikubwa, lugha inayotumiwa.

Mahakama nyingi nchini, hasa katika ngazi za chini na za kati, hutumia Kiswahili kwa kiwango kikubwa kuendesha shughuli zao.

Mashahidi wengi huwasiliana kwa Kiswahili—ama moja kwa moja au kupitia mkalimani. Kwa msingi huu, umahiri wa lugha ni hitaji la msingi.

Hata hivyo, katika mahojiano yanayoendelea ya kuwatafuta majaji wa Mahakama ya Rufaa, Kiswahili kinaonekana kupewa nafasi ya pembeni kana kwamba hadhi yake ni ya mapambo.

Inashangaza, basi, kwamba katika mchakato wa uteuzi wa majaji, lugha inayobeba sauti ya wengi inaokana kutothaminiwa ipasavyo.

Mahakama ya Rufaa si chombo cha kifahari cha kisheria pekee; ni nguzo ya haki inayopitia rufaa kutoka mahakama za chini—mahakama ambazo, kwa uhalisia, hufanya kazi katika mazingira ya Kiswahili kwa kiwango kikubwa.

Je, ni mantiki gani ya kuwa na majaji wanaokata rufaa za mashauri yaliyosikilizwa kwa Kiswahili ilhali wao wenyewe hawapimwi ipasavyo katika umahiri wa lugha hiyo?

Isitoshe, Kiswahili ni mojawapo ya masomo yanayozingatiwa wakati wa mwanafunzi kujiunga na masomo ya uanasheria.

Hii ni ishara tosha kwamba, mfumo wa kisheria unatambua umuhimu wa lugha hii katika safari ya taaluma ya sheria.

Ikiwa Kiswahili ni muhimu kujiunga na uanasheria, mbona kipuuzwe katika kupanda ngazi kwenye taaluma hiyo hiyo?

Kenya haiwezi kujinasibu kama taifa linalothamini urithi wake wa lugha huku ikiruhusu mifumo yake ya juu ya maamuzi kuendeshwa kana kwamba lugha za wananchi wake ni duni.

Kiswahili ni lugha ya kuunganisha, lugha ya taifa inayovuka mipaka ya kikabila na kijamii. Kukipa nafasi ya pembeni katika uteuzi wa majaji ni kuudhalilisha utaifa wetu.

Mwandishi ni msomi wa Kiswahili, mtafiti, mtafsiri na mkalimani