Maoni

Maoni: Kuondoa masharti ya vitambulisho mpakani hatari kwa usalama wa taifa

Na  BENSON MATHEKA February 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

TANGAZO la Rais William Ruto kwamba watu kutoka jamii zinazoishi katika kaunti za mipakani hawatawekewa masharti makali wakiomba vitambulisho vya kitaifa linaweza kuathiri pakubwa usalama wa kitaifa.

Masharti hayo na utaratibu ambao tangazo lake linafuta, yaliwekwa ili kuzuia watu kutoka nchi jirani, baadhi wakiwa wahalifu, wasipate vitambulisho vinavyoweza kuwasaidia kuishi na kuendeleza vitendo vyao nchini ikiwa ni pamoja na kuharibu na kupora mali na kisha kuipeleka katika nchi jirani.

Waliotuma vitambulisho vya kitaifa walikuwa wakipigwa msasa ili kubaini iwapo ni raia halisi wa nchi hii na hii haikufurahisha baadhi ya watu. Hii ilinuiwa kulinda usalama wa taifa ambao tangazo la rais linaweza kuweka hatarini.

Majasusi wa nchi jirani wanaweza pia kutumia njia za mkato kupata vitambulisho vya Kenya na kukusanya habari muhimu wakisiwasilisha kwa serikali za nchi zao na hata makundi hatari ya kigaidi.

Upatikanaji wa vitambulisho unawezesha watu kupata kazi na hata kuchaguliwa kushikilia nyadhifa muhimu na inaweza kuwa hatari kwa nchi watu wasio raia halisi wakifanya hivyo wakiwa na nia mbaya.

Inashangaza kuwa wakati nchi zinaweka masharti makali katika maeneo ya mipakani, serikali ya Kenya inatenda kinyume kwa hatua ambazo zinaweza kuruhusu wageni kupata uraia wa nchi hii.

Ni lazima kuwe na mfumo wa usalama kuzuia raia wa nchi jirani baadhi ambazo zinakumbwa na machafuko kupata stakabadhi za uraia za Kenya.

Mfumo huu, unapaswa kusukwa ili kuhakikisha raia halisi wa Kenya hawabaguliwi na hii inawezekana kwa kufuatilia kila mtoto anayezaliwa Kenya badala ya kufungua milango kwa kila mtu anayeomba kitambulisho kukipata.

Usalama wa taifa unafaa kupatiwa kipaumbele kuliko malalamishi ya kundi la watu ambao huenda wakawa na nia fiche. Kila ombi la kupata kitambulisho linapaswa kushughulikiwa kivyake.