Maoni

MAONI: Kwa IShowSpeed, Ruto amegundua siri za Gen-Z; atawadhibiti

Na DOUGLAS MUTUA January 19th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

HII ni makala maalum kwa watu ambao hawampendi Rais William Ruto. Ni vyema ukajua mapema unayekabiliana naye ni mtu sampuli gani.

Nakumbuka nikiandika kwenye ukurasa huu kwamba nchini Kenya kuna ulimwengu wa siri ambao Wakenya wengi hawajui upo, na wengi wanaoishi huko ni vijana.

Niliandika hayo baada ya kile kisa ambapo maelfu ya vijana walijitokeza nje ya Jumba la Mikutano ya Kimataifa (KICC) jijini Nairobi ili kusajiliwa kufanya kazi na kampuni ya kigeni ambayo wengi wetu hatukuifahamu kabla ya hapo.

Kwa ajili ya kumbukizi zako tu, usajili huo wa kipekee ulizuga akili za wengi kwa sababu, badala ya kutumia alama za vidole, mboni za macho zilitumika kumpa kila msajiliwa utambulisho maalum.

Lililowashangaza wengi zaidi ni kwamba mtu, au kundi la watu, liliweza kunadi na kuvumisha shughuli hiyo mbali na vyombo vya kawaida vya habari au mbinu nyinginezo tunazojua za kueneza matangazo ya kibiashara, watu wakashawishika kujitokeza.

Serikali ilifutilia mbali shughuli hiyo baada ya watu kulalamika.

Mambo yalitulia kwa muda, kisha ghafla maandamano ya Gen-Z yakatokea na kutushangaza sote, ispokuwa Gen – Z wenyewe, kwa jinsi walivyopanga mambo yao kisiri yakapangika bila ya kugunduliwa na makachero wa Idara ya Upelekezi wa Jinai (DCI).

Na bila shaka mwaka jana uliona vijana walivyoonyesha uwezo wao wa kujiandalia shughuli kubwa ya kitaifa bila kugunduliwa na vyombo vya dola pale walipojipanga na kuandamana ili kupinga mauaji ya mmoja wao, Mwalimu Albert Ojwang, nchi ikajaa taharuki.

Hayo ni matukio matatu makuu ambayo hakika yalimshangaza karibu kila mtu, hata Dkt Ruto mwenyewe, lakini nadhani alijifunza kitu fulani na kujiapia kuwa hatafumaniwa tena!

Hivi majuzi Wakenya wengi wameburudishwa na bingwa wa maonyesho ya tovuti ya YouTube na mitandao mingineyo ya kijamii kutoka Amerika, IShowSpeed (jina halisi, Darren Jason Watkins Jr.) katika hafla iliyowashangaza wengi kwa jinsi ilivyohudhuriwa na umati wa watu!

Kiongozi wa nchi mwenyewe alitufumania mara hii kwa kurekodi na video kisiri, ambayo kwayo alimkaribisha IShowSpeed nchini Kenya.

Wizara ya Utalii ilishiriki mipango hiyo kisiri pia, ikahakikisha utalii wetu umetangazwa vilivyo siku ya burudani hiyo.

Sasa ni dhahiri kwamba Dkt Ruto yuko, au anawakilishwa, kwenye mikutano ya siri ambako mambo yanapangiwa mbali nasi, hivyo itakuwa vigumu kumvizia kwa vyovyote vile kama awali.

Douglas Mutua ni mwanahabari Mkenya anayeishi Amerika ([email protected])