MAONI: Maadhimisho ya Saba Saba hayakuhitaji maandamano
JUMATATU iliyopita taifa letu liliadhimisha miaka 35 tangu kuanzishwa kwa maandamano ya tarehe saba Julai yaliyoasisiwa mnamo 1990.
Siku hii almaarufu Saba Saba, ni siku ambayo huadhimishwa kila mwaka nchini. Ni siku muhimu sana katika historia ya demokrasia ya Kenya.
Siku hiyo wanasiasa wenye maono na wanaharakati waliongoza hamasa ya kushinikiza kubadilishwa kwa kipengele cha 2A cha katiba ya zamani iliyoitambua nchi ya Kenya kuwa na mfumo wa chama kimoja.
Licha ya hayo wazalendo hao walitaka kuwepo kwa uhuru katika uchaguzi na kuidhinishwa kwa sheria inayoruhusu demokrasia ya vyama vingi.
Kama yalivyo maandamano ya siku hizi, waandamanaji wa Saba Saba walikabiliwa kimabavu na polisi. Baadhi yao walikamatwa, kuumizwa na wengine kupoteza maisha yao.
Baadaye, mnamo mwaka 1991, sheria ya chama kimoja iliondolewa na Kenya ikawa na mfumo wa vyama vingi vya kisiasa. Vyama vipya viliundwa na safari ya mageuzi zaidi ya kidemokrasia kuanza.
Mafanikio ya Saba Saba hayakukomea hapo,uhuru wa vyama vya kisiasa uliendelea na demokrasia ikazidi kukumbatiwa na wananchi pamoja na serikali.
Kuwepo kwa demokrasia ndiko kulikochangia taifa letu kuwa na katiba ya mwaka wa 2010 inayotumika kuongoza nchi yetu leo hii.
Ilivyowagharimu wananchi hata uhai wao, Saba Saba ya mwaka huu na nyakati zijazo tena haifai kuadhimishwa kwa maandamano.
Maadhimisho hayo hayastahili kutumika na wanasiasa wanaoipinga serikali kutishia usalama wa nchi bila ajenda maalum.
Ni kweli taifa hili lingali linakukumbana na ukiukaji mkubwa wa demokrasia kinyume na tulivyodhani. Hata hivyo, tunafaa kutafakari kwa undani na kujiuliza iwapo tunaitumia haki ya kuandamana visivyo.
Mwananchi anapoandamana siku ya Saba Saba anadai nini? Wananchi wanapofanya mandamano kila uchao bila kutofautisha kati ya maadhimisho na maandamano wanaisaidiaje nchi?
Huenda kuna msukumo mwingine hatari ama kuna mkono fulani wa kisiasa wenye nia ya kuichoma nchi. Huenda muda hautapita sana kabla ya kuitambua nguvu hiyo endapo Wakenya hawatakuwa makini.
Waandamanaji wana uhuru wa kuandamana siku nyingine badala ya kuchanganya ghasia na makumbusho ya jitihada za watangulizi wetu waliopigania demokrasia.
Viongozi serikalini nao wamepoteza fursa nzuri ya kuonyesha uzalendo. Itakuwa bora zaidi endapo kila mwaka, wakati kama huu viongozi watafanya mkutano na wananchi kuwakumbusha hatua tulizopiga kidemokrasia na kuhimiza umoja na uzalendo.
Ni vyema kutafakari kuhusu mstakabali wa taifa hili kisiasa na kiuchumi. Kizazi hiki kina jukumu la kuendeleza taifa hili bila vurugu.
Hata unapoidai haki na uwajibikaji,utakapoipata baada ya nchi kuvurugika, hiyo haki inakufaidi nini? Mwananchi yeyote anayedai kutafuka haki naye pia ana wajibu wa kuifanyia nchi yake haki.
Tunapoharibu mali ya umma na kutatiza shughuli za uchukuzi na biashara eti kwa sababu tunaadhimisha Saba Saba,huko ndiko kupigania demokrasia?
Ni changamoto gani zinatatuliwa kwa kuwasha moto barabarani,kuchokoza walinda usalama na kuwaibia wenzetu wafanyibiashara?
Ni kweli Kenya ina changamoto nyingi lakini siku ya Saba Saba itumike kukumbuka mema yaliyotokana na maandamano hayo. Pengine Wakenya hasa vijana wangetenga siku nyingine ya kuandamana kwa kutaka kusikilizwa na serikali.
Changamoto zinazotukumba Wakenya sasa si lazima zikabiliwe kwa ghasia.
Polisi wanapozifunga barabara pia hawana tofauti na waandamanaji wanaosimamisha shughuli za wananchi wengine.
Idara ya usalama inastahili kufikiria upya namna ya kulinda usalama pasipo kutatiza shughuli za mwananchi.
Hamasa na maridhiano yanahitajika kati ya idara za usalama na wananchi ili kuafikiana njia mwafaka ya ya kutekeleza wajibu wao kikatiba.
Kama taifa tunafaa kusuluhisha shida zetu kwa kuwa na mazungumzo yatakayoleta mabadiliko bila kudunisha amani katika taifa letu.
Kila Mkenya akumbatie uzalendo na kutupilia mbali ubinafsi unaolemaza maendeleo na mshikamano wa taifa letu tukufu.
Jasho na dhiki za wazalendo wa Sabasaba zatosha kuivusha Kenya hadi ng’ambo ya pili ya demokrasia endelevu