Maoni

Maoni: Mabloga wapewe bunduki za kujilinda

Na DOUGLAS MUTUA October 4th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NAAMINI wanasiasa wanaotumia nguvu kuwakomesha watu wanaowakosoa wana sehemu yao mahsusi ndani ya jehanamu, labda inayowaka moto wa mawe usiozimika milele.

Pia, naamini wanasiasa wanaotumia nguvu kuwatesa na kuwaumiza watu wanaohakiki kazi zao ni wanyonge wasiopaswa kuwa popote karibu na uongozi.

Vile-vile, naamini mwanasiasa yeyote asiyeweza kuvumilia matusi, chuki, dhihaka na dharau za wananchi hafai kabisa kujiita kiongozi, heri aache siasa na kurejelea maisha binafsi alikotoka.

La ziada ni kwamba naamini wakosoaji wa wanasiasa – hasa wanyonge wasio na watetezi – wanapaswa kupewa silaha za kujilinda dhidi ya dhuluma za kuwaumiza na kuwaachia majeraha ya kudumu au kuwaua.

Hili la wanasiasa kuwa na ukiritimba wa matumizi ya nguvu halijawahi, na hakika halitawahi, kuniingia akilini kwa kuwa naamini wanapewa uwezo wasiostahili kuwa nao.

Natamani sana kuishi katika dunia ambapo kila mwananchi wa kawaida anawajibika kikamilifu, hawatukani viongozi wake kwa mazoea, anakosoa kwa kukosolewa na kusifia kwa kusifiwa.

Hakika, ningetaka viongozi wetu waheshikmiwe kwa kuwa nao pia wanabeba mizigo mizito ya jamii nzima, lakini ni jambo lisilowezekana kuwafunza watu wa kawaida adabu na uungwana.

Nakataa katakata kukubaliana na maoni kwamba wanasiasa ni wanyama wasio na mipaka wanapolipa kisasi dhidi ya watu wanaowakosea, eti sote tuwe waangalifu mno tunapowahakiki ili tusidhulumiwe.

Ukiwa kiongozi una dhamana ya kuwalinda na kuwatetea watu wote katika jamii – wazimu, wagonjwa, wanyonge, watundu, makasisi, waumini, makafiri, mahasidi wasio na sababu, na kadhalika.

Hakuna taifa la walokole wala waswalihina pekee, kila mtu ana maisha yake, kwa hivyo ni muhimu sana kabla ya mtu kuwa mwanasiasa ajue atawawakilisha wote hao apende asipende.

Juma lililopita nimetia dua bila kukoma, nikiomba madai ya matumizi ya nguvu yaliyotolewa dhidi ya Gavana wa Mombasa, Bw Abdulswamad Nassir, yasiwe kweli.

Hata sasa naomba sana iwe Bw Nassir anasingiziwa tu kuwa anahusika na unyama ambapo mwanablogu wa Mombasa, BJK, alilawitiwa na kufanyiwa madhambi mengine yanayoweza kuhusishwa na watu wasiowahi kwenda shuleni hata siku moja.

Inasemekana kwamba BJK alivamiwa na watu zaidi ya 20 waliomhadaa kwamba wangalimpeleka kwa Bw Nassir ili akaombe msamaha baada ya kumtukana Gavana huyo matusi ya nguoni, ila akaishia kuteswa na kuachwa hoi.

Bw Nassir amekanusha madai hayo, akatoa yak wake kwamba maadui zake wa kisiasa wamekula njama kumpaka tope, na kuwa atathibitisha hana hatia kabisa.

Naomba iwe hivyo kikweli, Mungu awe shahidi yake, na ikiwa alihusika yamkute ya kumkuta, alipie dhambi zake papa-hapa duniani.

Si kwamba nampenda Bw Nassir, mwenyewe hata hanijui. Dua zangu hizo zinatokana na yale matamanio ya kibinadamu ya kuishi katika jamii isiyo na bughudha wala fedheha kiasi hicho.

Aidha, nina matarajio fulani na Bw Nassir kwa kuwa ni mwana wa aliyekuwa waziri katika serikali ya mwendazake Daniel Moi, marehemu Shariff Nassir, kwa hivyo amejua maana ya ustaarabu na kukosolewa kisiasa tangu azaliwe.

Sitaki kuamini kwamba kiongozi, hasa wa kitaifa, anaweza kukosa utu kiasi cha kufanya mambo ya kukata maini yanayohusishwa na Gavana huyo.

Naelewa kwamba hata ametukaniwa mama na mke, matusi ya nguoni hasa yasiyoandikika hapa, lakini bado naamini ukomavu wake unapaswa kuwa katika ubora wa juu zaidi kuliko wanaomtukana. Akishuka kiwango, atukane pia. Basi!

La ziada ni kwamba Bw Nassir ana mafedha mengi tu, anaweza kumshtaki yeyote katika mahakama yoyote, hata ikibidi ile ya upeo wa juu zaidi.

Mtundu akitozwa dhamana ya laki moja tu atasota jela au afyate, hutawahi kumsikia tena! Hata hivyo, ukimsababishia majeraha ya kudumu, utaishi kujutia vitendo vyako milele mradi makovu angali nayo.

Kwa mwanasiasa au mtu yeyote aliyejaaliwa nafasi ya hali katika jamii kutumia nguvu na kumuumiza mkosoaji badala ya kuonyesha ustaarabu wa kuacha pesa zake zimtetee kupitia vyombo vya dola ni sawa na kumuua mbu kwa nyundo.

Anayetumia fimbo kumuua chawa aliyening’inia kwenye mapumbu yake hujihasi bila kukusudia, ila huishia kujuta maisha yake yote.

Nasisitiza wakosoaji wa wanasiasa wachunguzwe kikamilifu kuhusu historia zao za uhalifu, wakiwa safi wapewe bunduki za kujilinda. BJK angekuwa na bunduki hangekaribiwa na watesi hao, hivyo hangeishia kutendewa unyama aliokumbana nao.

Kuwapa bunduki ni kulinda na kutetea haki yao ya kusema mambo ambayo labda hatutaki kusikia, lakini ni vyema wakayasema kwa sababu hakuna Mkenya yeyote aliye na ukiritimba wa mawazo.

Kenya ina historia ndefu ya kuwaua watu kwa sababu za kisiasa, lakini hao ni wanasiasa wazito au watumishi wa serikali au wanahabari watajika.

Mazoea mapya ya kuwaua au kuwaumiza watu wa kawaida wanaoichangamkia teknolojia duni ya kuweza kutumia simu kusema mambo ya kuudhi ni mtindo uchwara wa kulaaniwa vikali na kila mtu.

[email protected]