Maoni

MAONI: Mafarakano kati ya serikali, wabunge afueni kwa raia

Na MARY WANGARI August 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAKENYA wanashuhudia nyakati za kushangaza sana huku tanzu mbili kuu za serikali zikiumbuana na kupimana ubabe peupe baada ya Rais Ruto kumwaga mtama na kusema wabunge wamevuka mipaka kwa ufisadi.

Kauli ya kiongozi wa taifa imevutia ghadhabu kutoka kwa mabunge yote mawili nchini, Bunge la Kitaifa na Seneti, huku wabunge na maseneta wakitishia kumtimua rais.

Ukweli mchungu ni kwamba vitisho vyao vitasalia kuwa hewa na hawatofanya lolote kwa sababu walikubali tangu mwanzo kuingiliwa na serikali katika utekelezaji majukumu yao kwa raia.

Hali kwamba tawi la utawala linaloongozwa na rais sasa linakwaruzana na tawi la uundaji sheria huenda ikawa baraka kwa Wakenya ambao kilio chao kuhusu uwajibikaji kimeambulia patupu kwa miaka mingi.

Tawi la utekelezaji sheria kupitia idara ya mahakama limeangaziwa kwa sababu zote mbaya na kulaumiwa kwa kukosa kuwaadhibu wahusika wanaopatikana na hatia mbalimbali ikiwemo ufisadi, kupunja mali ya umma na maovu mengineyo.

Katika siku za hivi karibuni hata hivyo, bunge la kitaifa na seneti limemulikwa kwa kupitisha sheria zinazoonekana tu kuhifadhi maslahi yao ya kibinafsi na kupuuza zinazodhamiriwa kutatua changamoto anuai zinazowakumba wapigakura waliowachagua kuwaakilisha bungeni.

Imekuwa ada kwa sehemu kubwa ya wabunge kususia vikao vya kamati bila sababu thabiti na kugawanyika vibaya wakati wa kujadili masuala nyeti kama vile SHA na ufisadi uliokolea kupitia e-citizen.

Inapohusu kujadili masuala yanayowagusa kama vile kushinikiza SRC kuwaongeza mishahara na marupurupu, kuhalalisha NGCDF licha ya kutupiliwa mbali na korti au kubuni hazina ya malipo yao baada ya kustaafu, wabunge hujitokeza asilimia mia kwa mia na kuzungumza kwa sauti moja bila kujali nani anatoka kambi ya walio wengi au walio wachache.

Waziri wa Afya, Aden Duale, majuzi alifichua kwamba Sheria ya Tumbaku inayofanyiwa marekebisho ni moja kati ya sheria muhimu za kukomesha matumizi ya mihadarati na kulinda afya ya umma ambazo zimekaa bila kupitishwa kwa zaidi ya miaka saba, sababu kuu ikiwa wabunge kuingiliwa na mabwenyenye katika sekta hiyo.

Serikali na wabunge wameonekana kushirikiana kupendekeza, kubuni na kupitisha sheria tata zinazokusudiwa kuendeleza azma zao za kibinafsi licha ya amri ya korti huku Wakenya wakizidi kuumia.

Uhalisia ni kwamba japo tanzu hizi tatu za serikali zinapaswa kuwa huru na kutekeleza majukumu yake mahsusi bila hofu au kuingiliana kwa vyovyote, mambo ni kinyume.

Mafarakano kati ya serikali na wabunge huenda yakageuka baraka kwa Wakenya kwa kuimarisha uwajibikaji kutoka pande husika.