Maoni

MAONI: Masharti ya ODM yanazua hofu ya kisiasa ukanda wa Mlima Kenya

Na HELLEN NJAGI December 30th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

TUNAPOKARIBIA uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2027, ni wazi kuwa chama cha ODM kiko tayari kuendelea kuwa katika muungano wa Serikali Jumuishi na kuimarisha muungano huo ili uchukue uongozi wa urais katika uchaguzi huo.

Ikiwa hili litaafikiwa basi kuna uwezekano kuwa Naibu wa Rais Prof Kithure Kindiki hatakuwa mgombea mwenza Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu ujao.

Hili linajitokeza katika kauli za viongozi wa ODM ambao wanazidi kusisitiza kuwa iwapo chama hicho kitaendelea kuwa katika Serikali Jumuishi kwa lengo la kuunda serikali ijayo, sharti kuwe na mazungumzo ili kuwa na mkataba mpya kati ya ODM na UDA.

Kulingana na baadhi ya viongozi katika chama cha ODM, chama hicho kina wafuasi wengi wala hakiwezi kukubali kukaa katika Serikali Jumuishi hadi wakati wa uchaguzi ujao bila makubaliano yatakayokipa chama hicho nafasi zaidi za uongozi.

Wapo waliokiri kuwa sharti ODM ipate cheo cha naibu wa rais katika uchaguzi wa mwaka 2027.

Rais Ruto anaonekana kukubaliana na kauli za viongozi wa ODM anapowaambia kuwa yeye anaelewa siasa na chama cha ODM kinahitaji kujipanga naye atawapanga ‘wale wengine’ halafu watakutana waunde serikali pamoja.

Swali ni je, katika huko kuwapanga wale wengine Rais Ruto atakubali mapendekezo ya ODM ya kuteua naibu wa rais kutoka kwa chama hicho?

Ikiwa Rais atakubali mapendekezo ya ODM basi Prof Kindiki atakosa kuwa mgombea mwenza wa Rais Ruto katika uchaguzi mkuu ujao.

Ingawa Kindiki anaendelea kuimarika kama mwanasiasa mwenye ushawishi zaidi katika ukanda wa Mlima Kenya, eneo lililokuwa ngome ya Rais Ruto katika uchaguzi wa 2022, nafasi yake ya unaibu wa urais inahatarishwa na kuwa sasa Mlima Kenya umegawanyika kisiasa.

Ni bayana kuwa asilimia kubwa ya wapigakura kutoka Mlima Kenya ilimuunga mkono Rais Ruto katika uchaguzi wa 2022.

Kubanduliwa kwa aliyekuwa naibu wa rais Rigathi Gachagua mamlakani kumesababisha baadhi ya wapigakura katika ukanda huo kuunga mkono upinzani, jambo linaloponguza kapu la kura za Serikali Jumuishi katika ngome ya Prof Kindiki.

Ikiwa upinzani utaendelea kukita mizizi katika Mlima Kenya, huenda Rais Ruto akakosa kumteua Kindika kuwa naibu wake katika uchaguzi mkuu wa 2027 ili kumteua naibu rais kutoka ODM kwa lengo la kuungwa mkono na wafuasi wa chama hicho.

Prof Kindiki amekuwa ngao ya utawala katika serikali ya Rais Ruto. Kuteuliwa kwake kama naibu wa rais kulilenga kuimarisha uhusiano wa kisiasa wa eneo la Mlima Kenya na Rais Ruto hasa baada ya kumbandua Gachagua mamlakani.

Masharti ya ODM yanazua wasiwasi ya kisiasa Mlima Kenya na iwapo Prof Kindiki hatakuwa mgombea mwenza wa Rais katika uchaguzi ujao, huenda uhusiano huo ukapungua kwa kiwango kikubwa na ufuasi wa Dkt Ruto katika ukanda huo kudorora zaidi.