Maoni

MAONI: Mswada wa Fedha ulianika wabunge kuwa wasiosikiza wapigakura waliowachagua

Na MARY WANGARI July 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KATIKA kipindi cha majuma machache yaliyopita, Wakenya katika maeneo mbalimbali nchini wameshtushwa na hatua ya wabunge wao kuwaomba msamaha kwa kuunga mkono Mswada wa Fedha 2024 uliotupiliwa mbali.

Rais William Ruto alikataa kutia saini Mswada huo uliopendekezwa kufuatia maandamano yaliyoongozwa na vijana wanarika almaarufu Gen Z.

Baada ya Kiongozi wa Taifa kuchukua hatua hiyo, baadhi ya wabunge waliopiga kura kupitisha mswada huo Bungeni, walianza kurejea mashinani na kuwaomba msamaha wapiga kura.

Haya yalijiri huku raia wenye ghadhabu wakiteketeza na kuharibu mali inayohusishwa na wabunge wao waliohisi kwamba, wamewasaliti na badala yake kujali nafsi zao pekee.

Vijana waliwakosesha usingizi wabunge kwa kuwahangaisha kwenye mitandao ya kijamii na kupitia simu zao wakitumia kauli inayohofiwa mno ya “tumsalimie” katika juhudi za kutaka sauti zao zisikike.

Ni kwa sababu hiyo ambapo baadhi ya wabunge walinyenyekea na kuwaomba raia msamaha huku baadhi wakidai hawakuwa na hiari kupiga kura ‘ndio’ kwa sababu walitishiwa.

Hali hiyo ya wabunge kughairi nia ghafla na kuanza kukosoa Mswada waliopigia kura imeibua maswali na kufichua hali ya wabunge wanaotembea na upepo bila msimamo wowote.

Hata hivyo, kuna wabunge waliosimama imara na chaguo lao licha ya vitisho kutoka kila pembe na hatari ya kukosa kuchaguliwa tena kwa hatamu nyingine.

Baadhi ya wabunge hao wanatoka mrengo wa upinzani ambapo wanakabiliwa sio tu na tishio la kukosa kupoteza nyadhifa zao bali vilevile kuadhibiwa na vyama vya kwa kwenda kinyume na kambi yao.

Wabunge hao walistahimili cheche za matusi na masimango na kuwakabili kijasiri wapiga kura wakifafanua sababu zao za kupigia kura Mswada Fedha 2024 bila kumlaumu mtu yeyote na kujivunia chaguo lao.

Kutokana na ufafanuzi wao, ni bayana kuwa walichukua muda kusoma kwa makini Mswada huo kabla ya kufanya maamuzi waliyofanya na ndiposa hawakuchelea kutetea uamuzi wao.

Sifa mojawapo inayovutia kuhusu kiongozi yeyote, iwe ni katika familia, kampuni, timu ya spoti na jamii kwa jumla, ni kuwa na msimamo thabiti.

Kiongozi mwenye msimamo thabiti, kando na uwezo wa kufanya maamuzi muhimu kwa dharura, huvutia imani kutoka kwa wadogo na wafuasi wake wanaomwaminia mustakabali wao.

[email protected]