MAONI: Museveni hafai kuwania urais tena
SIKU moja, miaka kadha iliyopita, nikinyoosha miguu na kupiga soga jijini Nairobi na aliyekuwa mwandishi na mtangazaji maarufu, Ken Walibora, nilimuuliza kwa nini hakuwa amewasilisha makala na video zake wakati wa mashindano ya mwandishi bora nchini.
Marehemu Walibora, ambaye alikuwa ameshinda mashindano hayo mara kadha, alinitazama na kuniambia kuwa, kwa mujibu wa utamaduni wa alikozaliwa, mchezaji-ngoma hodari ni yule anayejua wakati wa kuondoka jukwaani.
Hakuwa na maana kwamba alinuia kuiacha kazi ya kuandika wala kutangaza, la hasha! Alinieleza kuwa aliona ni vyema mtu yeyote akitambuliwa kuwa stadi katika jambo lolote akawaachia na wengine ili wavume, kabla hajawachosha watu wakamkinai.
Hivi viongozi wa mataifa ya Afrika ni wachezaji-ngoma wasiojua wakati wa kuondoka jukwaani? Nimesalitika kuuliza swali hili baada ya kusoma habari za kuudhi na kutamausha: Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda ametia nia kuwania urais mwakani!
Hilo likitokea, mkongwe huyo ambaye atagonga umri wa miaka 81 mwezi Septemba mwaka huu atakuwa ameiongoza Uganda kwa miaka 40.
Kufikia sasa, Museveni, huku akiukana ukongwe na changamoto zake kwenye akili za binadamu, amebadili Katiba ya nchi hiyo mara mbili ili aruhusiwe kutetea wadhifa huo.
Mwanzoni mwa utawala wake, alinukuliwa akisema kuwa mtu yeyote aliyetimu umri wa miaka 70 hana uwezo wa kiakili wa kuitawala nchi.
Alibadilisha msimamo huo alipokaribia umri huo, kikawa kioja cha kweli ambapo viongozi fulani wa kidini walijitokeza na kumwonyesha kadi yake ya ubatizo iliyosahihisha tarehe yake ya kuzaliwa na kuonyesha kwamba alikuwa mchanga zaidi!
Sasa amegonga 80 na ushei, hawezi kuficha tena kwamba amekonga vilivyo, ila uchu wa mamlaka anao mwingi tu. Hajali iwapo akili zake zipo au la, umuhimu wa nchi kuongozwa na mtu aliyepevuka mawazo si muhimu tena, muhimu ni kudumu mamlakani.
Fununu kwenye shoroba za siasa zinasema kuwa, kutokana na umri na changamoto za afya, mzee huyo anafahamu fika kwamba huenda hana maisha marefu, lakini ameaminia kupanga urithi wa urais wake mwenyewe kabla hajafuata njia ya marahaba.
Haijulikani iwapo anataka kumrithisha mkewe, Bi Janet Kataaha Museveni, au mwanawe matata ajabu, Jenerali Muhoozi Kainerugaba. Mkewe ndiye waziri wa elimu na michezo, naye mwanawe huyo ndiye mkuu wa majeshi.
Zipo fununu nyingine zinazosema kwamba Mzee Museveni anashurutishwa na familia yake kudumu mamlakani ili wao wenyewe wajiandae vyema kumrithi akiwa angali hai ili wakitofautiana awapatanishe.
Haijalishi watalana maini au figo wakiwana kumrithi dikteta huyo, muhimu zaidi ni kujiuliza taifa la Uganda litabakije akiondoka hata leo hii ilhali hajamwandaa mrithi bora mwenye tajiriba ya kuiepushia nchi maafa yaliyonasibishwa nayo tangu mwanzo.
Rais Museveni na viongozi wengine wa mataifa ya Afrika wanaonata mamlakani wakipanga kuongoza milele wanapaswa kujua kuwa uhai hutoka kwa Mungu pekee, akikutaka leo ndio basi! Huagi hata jamaa na marafiki.
Wazee ving’ang’anizi waliokataa kung’atuka kama vile Paul Biya wa Cameroon, Paul Kagame wa Rwanda, Alassane Ouattara wa Ivory Coast, Salva Kiir wa Sudan Kusini na wengineo wanapaswa kuonyesha uzalendo kwa kuyaaminia mataifa yao kizazi kipya ili kiyaendeleze vyema zaidi wakiondoka mamlakani. Kurithisha jamaa zako si uzalendo, ni ubinafsi.
Wanapaswa kujifunza kuwa ujanja wao haufai kitu, mambo yanaweza kuwaendea visivyo ghafla. Wajifunze kwa kisa cha aliyekuwa rais wa Tanzania, marehemu John Magufuli, aliyepanga njama ya kumaliza upinzani na kubadili katiba ili awe rais wa maisha, pepo wa mauti akamzuru mapema.
Jenerali Omar al-Bashir, aliyeitawala Sudan (Khartoum) kama mali yake binafsi, hatimaye aligeuziwa na majeshi usiku wa kiza, akatiwa ndani, ambamo angali mpaka sasa, nalo taifa lake linamwaga damu kwa mazoea. Inamfaidije?
Kama mchezaji-ngoma hodari – samahani kwa kutaja uhodari na watu hao katika sentensi moja – viongozi wa mataifa ya Afrika wanapaswa kujua wakati wa kujiengua kabla hatujawakinai na kuwafurusha kwa mayowe na kero nyinginezo.
mutua_muema@yahoo.com