MAONI: Pima suti, harakisha fundi, Raila atatamba kura za AUC
WAKATI wa kampeni ya uchaguzi mkuu uliopita, wafuasi wa Kinara wa Upinzani Raila Odinga walikuwa na matumaini ya kuwahi urais kutokana na uungwaji mkono wa utawala wa wakati huo.
Kura ilipokuwa ikikaribia kauli kama ‘pima suti’ na ‘ambia fundi aharakishe’ zilitawala vinywa vya wafuasi wa Bw Odinga ambaye hadi baadhi ya waliorindima ngome yake wanaamini alishinda urais mnamo 2022.
Wiki hii, Bw Odinga atakuwa kwenye mizani, mara hii akilenga uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) ambayo uchaguzi wake unaandaliwa Jumamosi hii jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Wafuasi wa Bw Odinga wanaamini wadhifa huo una nguvu zaidi ya urais, kwa sababu, atakuwa akiwaongoza marais wengine Afrika na kushughulikia miradi mbalimbali pamoja na ushirikiano zaidi ya ukanda huu.
Binafsi na uchunguzi wa kina ambao nimeufanya, mara hii Bw Odinga anafanikiwa na wafuasi wake ambao hawajapima suti wamechelewa kwa hivyo waharakishe na wawatie mafundi presha.
Wiki ijayo, wakati kama huu, dalili zote zinaonyesha kuwa Raila atakuwa mwenyekiti wa AUC.
Atakuwa amewabwaga Mahmoud Ali Yossouf, Waziri wa Masuala ya Nje wa Djibouti na RichaRd Randriamandrato kutoka Kisiwa cha Madagasca.
Mwanzo, kama ni kampeni ya kuzuru na kuwashawishi Marais wa Afrika, Bw Odinga amewajibika. Kilichobakia sasa tu ni kulinda kura wala sina shaka kuwa AUC ina mifumo mizuru inayoeleweka ya uwazi uchaguzini.
Bw Odinga amekutana na karibu kila rais wa mataifa ya Afrika, akaeleza ajenda zake za kwa Afrika na kuomba uungwaji mkono.
Katika kila mkutano Kaskazini, Magharibi, Mashariki na Kusini mwa Afrika, alieleza ajenda yake kwa ukakamavu.
Pia amehudhuria mikutano ya Marais na makongamano ya Afrika na mataifa ya kigeni akiwa ameandamana na Rais William Ruto na kujipigia debe.
Ukilinganisha jinsi waziri huyo mkuu wa zamani amefanya kampeni na wapinzani wake, amekuwa bora zaidi.
Pili, Katibu Mkuu Moussa Faki anayeondoka anatoka Chad ambayo ipo kwenye ukanda wa mataifa yanayozungumza Kifaransa.
Ukiangalia AUC tangu ianzishwe ni Nkosazana Dlamini-Zuma ndiye anatoka mataifa yanayozungumza Kizungu aliyewahi kushikilia wadhifa huo.
Hata mtangulizi wa Bw Faki na Bi Zuma, Dkt Jean Ping, raia wa Gabon alikuwa akitoka kwenye nchi ambako inazungumza Kifaransa.
Kwa hivyo, itakuwa vigumu tena wadhifa wa AUC uendee Bw Youssouf ambaye pia anatoka nchi inayozungumza Kifaransa.
Tatu mataifa ya Uarabuni kama Misri, Algeria, Morocco yameonyesha kuwa yataunga mkono ‘Baba’ kwa sababu nao yanalenga kupata makamu mwenyekiti wa AUC.
Huu uchaguzi ni wa nipe nikupe na hilo huenda likamfaa na kiongozi huyo wa upinzani Jumamosi.
Pia hekima ambayo Rais Ruto ametumia kwa kushirikisha mataifa ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Mashariki (EAC) kushughulikia mzozo Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, pia imesaidia kuzima mgawanyiko ambao ungemharibia Raila kura.
Kama ni uzoefu Raila anao, kampeni nayo amepiga, kilichosalia sasa ni mfungo na dua wiki hii ili Jumamosi, ushindi uje nyumbani jinsi ambavyo wengi wanatarajia.
Tayari kitengo cha kampeni ya Bw Odinga imesema wana uhakika wa kupata kura 28 kwa hivyo, tano zilizosalia ili afike 33 zinazohitajika si ngumu.