MAONI: Polisi waheshimu haki ya upinzani kunadi sera zao
NI wajibu wa polisi kudumisha usalama nchini siku na saa zote.
Maafisa hao wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS), wanapaswa kuhakikisha kila Mkenya, bila kujali hadhi yake katika jamii, anapewa usalama.
Lakini inashangaza kuwa, maafisa wa polisi walionekana kujitia hamnazo Alhamisi alasiri genge la wahuni lilipovamia msafara wa magari ya wafuasi wa aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua aliporejea nchini kutoka nchini Amerika.
Wahuni walishambulia msafara wa Gachagua kwa mawe na silaha zingine butu katika barabara ya Mombasa Road karibu na mkahawa wa City Cabanas.
Watu kadhaa walijeruhiwa, wakiwemo wanahabari, na magari kuharibiwa kwa kuvunjwa vioo.
Inasitisha kuwa magari ya watu wengine ambao hawakuwa kwenye msafara huo wa viongozi na wafuasi wa Bw Gachagua, pia yalishambuliwa na wahuni hao walionekana kukodiwa.
Inaudhi kwamba siku moja baada ya kutokea kwa fujo hizo, Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen alielekeza kidole cha lawama kwa viongozi wa chama cha Democracy for the Citizen Party (DCP) akidai walifeli kujulisha maafisa wa polisi kuhusu barabara ambayo msafara wao ungepitia.
Bw Murkomen, ambaye alikuwa akiongea katika kaunti ya Kirinyaga, alidai kuwa serikali iliwaomba viongozi wa DCP kutoa habari kwa polisi kuhusu shughuli zao wakati wa kurejea nyumbani kwa Gachagua lakini wakakataa.
Kwa kweli maelezo hayo hayana mantiki yoyote kwa sababu malori ya polisi yalionekana barabarani kuanzia katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) hadi katika barabara ya Mombasa.
Waliwatazama wahuni walioshambulia msafara wa Gachagua karibu na mkahawa wa City Cabanas bila kufanya chochote.
Sasa Bw Murkomen anatoa ahadi hewa kwamba polisi wameanzisha uchunguzi kubaini wale ambao waliwakodisha vijana hao kuzua fujo kwa kushambulia msafara wa Gachagua, tukio ambalo lilisababisha uhabirifu wa mali.
Nasema ni ahadi hewa kwa sababu hii sio mara ya kwanza kwa Bw Gachagua na wafuasi wake kushambuliwa na wakora huku polisi wakitizama bila kuingilia kati.
Nakumbuka mnamo Novemba 26, mwaka jana, fujo zililipuka baada ya kundi la vijana kuwavamia waombolezaji katika hafla ya mazishi ambayo Bw Gachagua na wafuasi wake walihudhuria eneo la Limuru, kaunti ya Kiambu.
Licha ya kwamba vurugu zilinaswa kwenye kamera za wanahabari na baadaye kupeperushwa kupitia runinga za humu nchini, vijana waliotekeleza uhalifu huo hawajakamatwa.
Hilo halifai kamwe.