Maoni

MAONI: Rais bado ana muda wa kukomboa urithi wake, achape kazi tu!

Na KINYUA KING'ORI October 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MIAKA miwili inatosha kwa kiongozi mweledi kutimiza ahadi zake na kuchochea mafanikio na kuleta utulivu wa kisiasa katika nchi.

Sifa za kiongozi bora si wingi wa maneno, bali umahiri katika kutekeleza wajibu wake kwa kuhakikisha amewapa msisimko wananchi kwa kupuuza yale yasiyo muhimu na kulenga ustawi.

Utendakazi bora haupimwi kwa sifa na ujasiri wa ulumbi katika hafla za kisiasa au kuvuruga mafanikio yaliyoanzishwa na watangulizi.

Uongozi ni neema kutoka kwa Mola na haupaswi kutumiwa kubomoa mafanikio kiustawi, kisiasa na kiuchumi.

Sasa kwa vile Dkt William Ruto ndiye Rais, asiwe kiongozi wa kulalamikia kauli za upinzani za ‘Wantam’ bali asimame kidete na kukumbatia utawala bora wenye sera za kuvutia bila kudhalilisha katiba.

Vinara wa upinzani wanapokosoa ufisadi na utepetevu serikalini si eti kwamba wamekosea, wanatekeleza wajibu wao wa kikatiba.

Je, Rais anatarajia Rigathi Gachagua au Kalonzo Musyoka kusifia utendakazi bora serikalini?

Kwa nini Rais akoseshwe usingizi na maneno matupu ya ‘wantam’ ikiwa anayo miradi bora anayotekeleza katika kipindi hiki?

Hasira na presha za nini?

Katika uchaguzi ujao, raia watajiuliza kwa nini Ruto awe ni ‘Wantam’ au ‘Tutam’?

Je, alifaulu kutimiza ahadi zake na kuboresha maisha yao?

Maswali ni mengi na vijana wameamua watabadilisha mwelekeo wa siasa 2027 kwa kuonyesha ukomavu kwa kuchagua kiongozi mwenye maono na mipango bora kutatua changamoto zinazokumba sekta ya afya, elimu, sheria, usalama na ajira.

Rais usilaze damu. Bado anao muda wa kunyoosha mambo hadi akumbatiwe tena.