MAONI: Ruto achunge, ufujaji pesa utamfanya awe ‘Wantam’!
JUZI, kwa mara nyingine, Wakenya kwenye mitandao ya kijamii walielekezea hasira zao kwa hatua ya Rais William Ruto kukodi ndege ya kifahari kwa ziara yake nchini Ethiopia.
Hii ni kufuatia habari iliyochapishwa kwenye gazeti moja la humu nchini iliyoelezea kwa kina gharama ya ndege aina ya Gulfstream GV ambayo Dkt Ruto alitumia kwa safari hiyo.
Kulingana na wataalamu, gharama ya kukodisha ndege hiyo, inayosimamiwa na kampuni ya SkyMark Executive, ni kati ya Sh2.3 milioni hadi Sh3.3 milioni kwa saa moja.
Kwa upande mwingine, safari ya kati ya Nairobi na Addis Ababa, kwenda na kurudi inagharimu Sh179,730, kwa ndege za Shirika la Kenya Airways, kitengo cha watu mashuhuri.
Tangu habari hizo zitolewe kwa umma Jumanne wiki jana, Ikulu ya Rais haijatoa taarifa zozote za kupinga au kutoa ufafanuzi zaidi kuhusu suala hilo.
Hii ni tofauti kabisa na mwaka jana, 2024, ambapo Rais Ruto mwenyewe alijitokeza na kufafanua kwamba, safari yake nchini Amerika kwa ndege ya kifahari Boeing 737-700 iligharimu Sh10 milioni wala sio Sh200 milioni, pesa za walipa ushuru.
Akiongea Mei 26, wakati wa Hafla ya Maombi ya Kitaifa katika Safari Park Hotel, Nairobi, Rais alisema hivi: “Mimi sio mwenda wazimu bali kiongozi anayewajibika. Siwezi kutumia Sh200 milioni kwa safari ya Amerika. Serikali haikutumia zaidi ya Sh10 milioni kwa ziara hiyo.”
Lakini kwa mtazamo wangu, unafiki wa Rais Ruto ni kwamba, kila mara hutangaza taratibu za kupunguza gharama ya matumizi ya pesa za umma serikali lakini baada ya siku chache anakiuka taratibu hizo.
Baada ya maandamano ya Gen Z kati ya Juni na Julai 2024, Rais alitangaza mikakati kadhaa ya upunzaji gharama kama vile kupunguzwa kwa safari za maafisa wa serikali, kupunguzwa kwa idadi ya washauri katika afisi yake na afisi za mawaziri, matumizi ya majengo ya serikali kwa mikutano wala sio mikahawa ya kibinafsi miongoni mwa hatua nyinginezo.
Sababu ni kwamba, mojawapo ya maovu serikalini ambayo vijana hao wa kizazi cha sasa walikuwa wakilalamikia ni ubadhirifu wa pesa za serikali ilhali wao wanazongwa na mseto wa shida.
Kwa mfano, vijana walikerwa na mienendo ya wakuu serikalini na wandani wa Rais Ruto kutoa mamilioni ya pesa katika harambee ilhali miradi na mipango muhimu ya serikali inakosa pesa.
Inavunja moyo kwamba baada ya mambo kutulia na Rais Ruto kubuni ushirikiano wa kisiasa na kiongozi wa ODM Raila Odinga, ubadhirifu wa pesa za umma umerejea kwa kishindo.
Dkt Ruto anapojipiga kifua akisema ndiye anapasa kuchaguliwe tena 2027, ajue kwamba huu ubadhirifu wa pesa za umma utamzuia kufikia lengo hilo.