MAONI: Ruto anajitia kwenye tanuri la moto kisiasa kwa kuendelea kusuta kanisa
RAIS William Ruto hafai kuendelea kulumbana na viongozi wa makanisa wakiwemo maaskofu wa Kanisa Katoliki ambao majuzi walijitokeza kwa ujasiri na kulaumu serikali yake kwa kufeli kuwajibikia ahadi zake kwa Wakenya na kufaulu katika vita hivyo.
Rais hana budi kubadilisha mbinu zake za utawala na mikakati yake katika juhudi za kutimiza ahadi zake badala ya kujitia katika tanuri la moto kisiasa kulumbana na maaskofu ambao si wanasiasa. Kile wanachotekeleza ni wajibu wao muhimu wa kufichua maovu serikalini.
Raia kwa sasa wamezongwa na mawazo huku familia zingine zikilala njaa kwa ukosefu wa chakula kutokana na hali mbaya ya uchumi katika taifa letu. Je,ni kanisa linalostahili kuwajibika kwa kufeli kwa mfumo wa ufadhili wa elimu ya vyuo vikuu na matatizo sugu yanayotatiza Bima ya Afya ya SHIF au ni Rais na serikali yake ya Kenya Kwanza?
Viongozi wa makanisa na waumini wao ni raia waliompigia Rais kura. Hivyo, ni aibu kuwakosoa wakati wanadai serikali imeshindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo kwa uaminifu, usawa na kuzingatia katiba.
Inawezekana Rais Ruto hajui matatizo yanayotatiza raia maskini na jinsi wanavyochukia utawala huu kwa kuendeleza ukabila, ufisadi, utekelezaji duni wa maendeleo na sera kandamizi zinazowaumiza watu?
Mbona sasa anawasuta maaskofu ambao wamemwambia ukweli ambao vibaraka wake hawawezi kumwambia kuwe usiku au mchana? Anasahau vipi haraka siku ambapo waumini walishangilia ushindi wake kwa kauli mbiu ya ‘Ni maombi si uchawi’? Hajui kwamba huenda kibwagizo kibadilike kufikia mwaka wa 2027?
Rais angelizingatia ushauri wa maaskofu, angeepuka ghadhabu ya wakazi Embu. Hangejinata kwa kuzungumzia ‘ufanisi’ wa Bima ya SHIF katika hotuba yake iliyowakera raia wengi wanaokosa matibabu.