Maoni

MAONI: Ruto kutaka Raila ashinde kura kule Addis Ababa ni kwa faida yake binafsi

Na PAUL NABISWA February 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KATIKA mkutano wa maombi ya Raila Odinga uliofanyika jijini Nairobi, hoja kuu aliyotoa ‘baba’ ni kwamba, akishinda uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, atafurahi na pia akishindwa hatalia.

Huu ulikuwa ujumbe mzito kwa wafuasi wa Raila na serikali ya Rais Ruto ambayo imo mbioni kuhakikisha Raila anasalia Addis.

Zipo sababu maalumu za kutaka Raila ashinde hicho kwa kinyang’anyiro japo anakabiliwa na ushindani mkubwa kutoka kwa mgombeaji kutoka Djibouti Mohamoud Youssouf.

Akishinda, itamaanisha kuwa Ruto hatakuwa na wasiwasi wa kukabiliana na Raila katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Ikiwa marais wa Afrika hawatampa ridhaa ya kuongoza shughuli zao za kisera barani Afrika, hewa ya siasa itachafuka.

Raila alimwokoa Ruto kutokana na wimbi kubwa la Gen – Z. Ruto akabuni ile serikali “jumuishi” na kuwaingiza serikalini wakuruba wa Raila.

Ikiwa atapoteza inaashiria nini? Je, Raila atatulia na kutazama siasa za Kenya kwa umbali?

Akiamua anarudi uwanjani hawa “watu wake” walioteuliwa serikalini watavumiliwa na Ruto ama tutaona tena mabadiliko ya ghafla katika baraza la mawaziri?

Dalili za mpasuko katika ODM zinatakiwa kumtia wasiwasi Raila na hata Rais William Ruto bila kujali ikiwa Raila atashinda kiti cha AUC na vinginevyo.

Kwa mfano, Gavana James Orengo ameweka hadharani kuwa nyadhifa muhimu bungeni za Muungano wa Azimio zinatakiwa kupewa viongozi wake kwa kuzingatia maamuzi ya mahakama.

Si hayo tu, hatua ya viongozi wa ODM akiwemo naibu kiongozi wa chama Simba Arati kuunga mkono msimamo wa katibu mkuu wa ODM Seneta Edwin Sifuna ni dalili kuwa chungwa linazidi kuwa chungu.

Orengo na Sifuna katika hafla tofauti, na si mara moja wamesema kuwa, serikali ya Kenya Kwanza inataka kutumia nafasi ya Raila ya AU kuficha maovu yake.

Katika mazishi ya aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Haki za binadamu Roseline Odede, Orengo aliitaka ODM kuwa makini isije ikatumiwa vibaya kuweka muhuri kile alichotaja kuwa maovu kama vile utekaji nyara wa vijana miongoni mwa mambo mengine.

Naye Sifuna akasema “Baba, watoto wa watu wanatekwa nyara, wanapotea na hawapelekwi kortini, nikisema haya maneno watu wanasema, nyamaza, utaharibia baba kura ya AU.”

Ikiwa Raila atafaulu, itakuwa fahari kubwa kwa Kenya na pia itatoa nafasi kwa wanasiasa wengine kujitokeza na kuuza sera zao Raila akitazama kwa mbali matukio nchini.

Pia utakuwa mtihani mkubwa kwa watu wenye fikra za kimapinduzi ambao walikuwa chini ya baba na wakaogopa kutamka kuchunguza ikiwa watasema ya kwao ama watasubiri baraka za baba.

Ni siku chache tu na atajulikana baba wa AUC.