MAONI: Tiketi ya Kalonzo-Matiang’i ndiyo bora kwa upinzani
BADALA ya kuandaa vikao vingi vya kunywa chai na kushauriana, viongozi wa upinzani wanastahili kuamua mwaniaji wao wa urais mapema.
Ukitathmini viongozi wote wa upinzani, basi utashawishika kuwa tiketi pekee ambayo itakuwa bora zaidi ni Kalonzo-Matiang’i.
Yaani Kalonzo Musyoka awanie urais kisha aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i awe mgombeaji mwenza.
Ni tiketi ya Kalonzo-Matiang’i ndiyo angalau inaweza kumtoa jasho Rais William Ruto ila nao itabidi wafanye kazi ya ziada kuhakikisha wanapata ushindi.
Kwa muda sasa, viongozi wa Upinzani wamekuwa wakiandaa tu vikao vya kunywa chai na kupiga gumzo badala ya kujizatiti kusaka mgombeaji bora kati yao na kumtangaza kwa wafuasi wao.
Wiki mbili zilizopita, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua alinukuliwa akisema kuwa naye bado anaweza kuwania urais 2027.
Alidai kuwa kesi aliyowasilisha mahakamani kupinga kung’atuliwa kwake uongozini bado haijaamuliwa kwa hivyo hawezi kuzuiwa kuwania urais.
Bw Gachagua alijinaki kuwa ana uungwaji mkono wa kutosha na uwezo wa kumwaangusha Rais Ruto.
Alitaja hatua ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta na Ruto kuwania urais 2013 licha ya kuwa na kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).
Vilevile, alimtaja mbunge wa Sirisia John Waluke ambaye alihukumiwa kifungo cha miaka 74 lakini bado akawania na kushinda ubunge mnamo 2022.
Hoja ya Bw Gachagua ni kwamba kesi yake haijasikiziwa na kuamuliwa wala hata haijafika Mahakama ya Rufaa na ya Juu kwa hivyo yuko huru kuwania.
Haya ya Bw Gachagua ni vitimbi kwa sababu hawezi kuidhinishwa kuwania uongozi wa nchi ilhali katiba ilifuatwa katika kumngóa madarakani.
Uhuru, Ruto na Waluke hawakung’olewa madarakani na bunge.
Badala ya vishindo hivi, Bw Gachagua anastahili kuunga mkono tiketi ya Kalonzo-Matiangí na kupambana ipate ushindi ndipo naye anufaika hata akiwa nje ya uongozi.
Mwanzo, Kalonzo, 71 atakuwa 73 kufikia 2027 na iwapo ataighairi nia yake ya kuwania urais mara hii, atakuwa na umri wa miaka 78 mnamo 2032.
Kuna wanasiasa wengi wanaochipuka katika ngome yake ya upinzani ambao wamechoshwa na tabia yake ya kuwaunga wengine tangu 2013 na wanaiona 2027 kama mwaka wake wa kuingia ikuluni.
Pia, ameapa mara kadhaa kuwa 2027 hatamuunga mkono mgombeaji mwengine, kwa hivyo ni bora iwapo atapewa nafasi na upinzani.
Halafu, akilinganishwa na viongozi wengine ndani ya upinzani, Bw Musyoka anaonekana kama kiongozi wa kitaifa na chama chake cha Wiper kina sura pia ya kitaifa kando na kuwa na ufuasi sana Ukambani na baadhi ya maeneo ya Pwani.
Dkt Matiang’i naye bado hajaiva sana kuwa rais japo anashabikiwa sana na Gen-Z kutokana na uchapakazi wake alipokuwa serikalini.
Kadhalika, akifanikiwa kupata uungwaji mkono wote wa Gusii, basi atanufaikia kura ambazo zimekuwa zikiendea sana Kinara wa Upinzani Raila Odinga kwenye chaguzi zilizopita.
Tiketi ya Kalonzo-Matiang’i kisha nyadhifa nyingine kubwa ziendee Magharibi na Mlima Kenya kutahakikisha kuwa wanafanya iwe vigumu kwa Rais Ruto kuwahi awamu ya pili.
Kumtaja mgombeaji 2026 kutakuwa kumechelewa sana kwa kuwa wakitambulishwa sasa watakuwa na mwanya wa kukabili mgawanyiko ambao utazuka kati yao kutokana na uamuzi huo.