MAONI: Trump amejibwaga kwenye tanuri la moto kwa kutishia bilionea Musk
MCHEKESHAJI maarufu zaidi wa Afrika Kusini anayeishi Amerika, Trevor Noah, aliwahi kusema kuwa Rais Donald Trump ana tabia za viongozi dhalimu wa Afrika.
Msanii huyo aliyepata umaarufu kwa kuwacheka na kuwachekesha Waamerika aliorodhesha mambo ambayo kwayo Trump na viongozi wengi wa Afrika wanafanana, wakati wa utawala wa kwanza wa Trump, ikachukuliwa kama mzaha.
Hata hivyo, kauli yake hiyo inaendelea kudhihirika wakati huu ambapo Trump anaongoza kwa muhula wa pili kwa kuwa mambo hayo – kama vile uchu wa mamlaka, kutishia kuwaadhibu wapinzani wake na kuyatumia majeshi visivyo – yanatimia.
Unaposoma makala hii, kiongozi huyo wa taifa lenye nguvu zaidi duniani anatishia kuwafurusha kutoka Amerika wazaliwa wawili wa Afrika, ambao wametokea kutamba si haba na kuwapiku Waamerika wengi kwa biashara na siasa.
Trump ametishia kumfukuza Bw Elon Musk, mzaliwa wa Afrika Kusini ambaye ndiye tajiri mkubwa zaidi duniani wakati huu.
Pia, rais huyo ametishia kumkamata na kumfukuza Bw Zohran Mamdani, 33, mzaliwa wa Uganda ambaye anawania wadhifa wa meya wa jiji la New York.
Vita vya maneno kati ya Trump na Musk vinavyoendelea mtandaoni vinawaburudisha wengi mno, hasa ikizingatiwa kuwa wana ushawishi mkubwa kwenye mitandao ya kijamii wanayomiliki.
Huku Trump akitumia Truth Social kujigamba anavyoweza kumpokonya Musk fursa za biashara, kumvua uraia wa Amerika na kumrejesha Afrika Kusini, mmiliki huyo wa X anamwambia athubutu aone cha moto!
Wawili hao, ambao hadi hivi majuzi tu walikuwa washirika wa karibu, wametofautiana kuhusiana na ukusanyaji ushuru na matumizi ya pesa za serikali.
Kampuni nyingi za Musk zinapokea mabilioni ya dola za serikali kama msaada unaopewa mashirika binafsi ili yaendelee kuwekeza nchini Amerika na kubuni fursa za kazi, mpangilio ambao umemwezesha kuwa na utajiri mkubwa zaidi duniani.
Trump anatishia kupunguza msaada huo na kumfukuza Musk Amerika, naye Musk anamwambia auondoe kabisa kisha ajiandae kuondolewa mamlakani kwa kura za wabunge!
Trump akitekeleza tishio hilo litaathiri uchumi wa Amerika kwa kiasi kikubwa kwani Musk anaweza kuhamishia kampuni zake kwingineko, na bila shaka Kenya itaathirika kwa kuwa Musk ndiye mmiliki wa kampuni ya huduma za intaneti ya Starlink.
Trump anatishia kumrejesha Bw Mamdani Uganda kwa kisingizio kwamba mwanasiasa huyo mchanga hakuifahamisha idara ya uhamiaji kuwa anaunga mkono ugaidi alipohojiwa kwa ajili ya kupewa uraia wa Amerika.
Dai hilo la kuunga mkono ugaidi linatokana na msimamo wa Bw Mamdani wa kuunga mkono uhuru wa Wapalestina, jambo linalochukuliwa kuwa anatishia taifa la Israel.
Nimekiita kisingizio kwa sababu naamini Bw Mamdani analengwa kwa kuwa ni mwanasiasa wa chama cha upinzani cha Democrat kinachomkosoa Trump vikali kila wakati. Angesazwa angekuwa mwanachama wa Republican, anachoongoza Trump.
Matishio hayo ya Trump yananikumbusha enzi ya marehemu John Magufuli, ambaye wakati wa utawala wake aliwasingizia makosa ya kuwa raia wa nchi nyingine Watanzania waliomkosoa vikali.
Hivyo ndivyo Magufuli alivyowanyamazisha wanasiasa, wanahabari na wanaharakati waliojasiria kuhakiki sera na dhuluma za serikali yake.
Barani Afrika, hasa ikiwa unatokea eneo la mpakani, ukimkosoa kiongozi wa nchi tu unatishiwa kwamba utapokonywa uraia na kurejeshwa nchi inayodhaniwa kuwa yako.
Aghalabu unapata watu wanaotokea maeneo ya mipakani hawaaminiwi kabisa na serikali, wanapewa vitambulisho vya kitaifa kwa masharti, na kamwe hawapati kazi muhimu serikalini.
Ni kosa kutumia suala la uhamiaji kuwanyamazisha watu. Bila shaka Musk na Mamdani, hata wakifukuzwa Amerika, wanaweza kuishi kokote kwingineko duniani, lakini raia wa kawaida akikabiliwa na tishio hilo atahofia kukosa mahali kwa kuita nyumbani.
mutua_muema@yahoo.com