MAONI: Trump ananishangaza, ana tabia za kiongozi Mwafrika!
HIVI umewahi kuambiwa kitu na mtu, mwanzo ukakubaliana naye mia kwa mia, ila baada ya kutafakari kidogo ukatanabahi kuwa uliokubaliana nao si ukweli wa mambo?
Hivi majuzi nimepeleka gari langu kufanyiwa ukaguzi wa kiusalama kama ilivyo ada kwenye nchi ya watu ninakoishi – Amerika.
Na kwa kuwa nilihitaji kufanya mambo mawili-matatu sehemu mbalimbali, ilibidi niabiri Uber.
Kawaida yangu ninapokutana na watu –labda kutokana na mapenzi yangu ya siasa au udarai wa kawaida wa mwanahabari tu –napenda kuanzisha mazungumzo ya jumla kuhusu masuala ibuka.
Mara hii nilimuuliza dereva wa Uber anavyoona mambo yakiendelea Amerika chini ya utawala wa Donald Trump, mkorofi ambaye anawahangaisha watu wasio wazawa wa Amerika, hata waliopata uraia kihalali.
Dereva, ambaye ni raia wa Amerika ila mwenye asili ya Ghana, alipaaza sauti: “Ala! Mbona umeamua kuniuliza kuhusu mtu huyo mgonjwa anayevuruga mambo? Kawaida yetu Waafrika hatuwachukii wala kuwahukumu wagonjwa, lakini huyu amezidi sana.”
Amezidi vipi? Nilimuuliza, naye akajibu, “Kwa chuki, ubaguzi wa rangi na uvunjaji sheria kiholela tu kana kwamba hajui nchi hii ina Katiba.”
Aliendelea, “Nakuapia Jalali, ingekuwa Afrika, mtu huyu hangechaguliwa chochote, acha urais tu! Kwetu Afrika, huyu hawezi kupata ubunge wala udiwani. Kashfa zake nyingi, miongoni mwazo hukumu za mahakama zilizothibitisha ni mhalifu – zingemponza hata asithubutu kuwania wadhifa wowote.”
Maneno yake hayo yalinichangamsha, nikakubaliana naye kwa asilimia zote, sikwambii na nikaanza kuuonea fahari Uafrika wangu.
Nilimwambia dereva huyo kuwa kwa kweli watu wa mabara mengine wamezoea kuidharau Afrika, lakini matendo ya Trump yamedhihirisha kuwa heri sisi.
Kwa nini nikawa na msimamo huo? Kikawaida, hata viongozi wa mataifa wakiwatawala watu kimabavu, watawala wenyewe na wanaotawaliwa wanajua watawala hawana dhamana wala ridhaa ya wananchi.
Wanatawala kwa kifua, mpende msipende.
Tofauti na Amerika? Raia wa taifa hilo tajiri na lenye nguvu nyingi zaidi za kijeshi duniani waliamka na kuelekea katika vituo vya kupigia kura, wakamchagua Trump, mhalifu aliyekutwa na hatia katika makumi kadha ya mashtaka ya jinai.
Nilipofika sehemu niliyokusudia kwenda niliteremka kutoka Uber ya watu, nikampa mkono dereva, nikampongeza kwa kuwa na akili pevu, nikamhimiza asilegeze msimamo na mtizamo huo.
Muda si muda, nilianza kutafakari kuhusu mazungumzo yetu. Hiyo huwa kawaida yangu kila ninapojipata nikikubaliana na watu kuhusu kila jambo.
Nilijiuliza: Hivi kweli Trump ni mbaya hivi kwamba sheria pamoja na Waafrika hawangempa urais? Je, ni kweli kwamba Waafrika ni watu wazuri na werevu kuliko Waamerika, eti hawawezi kumchagua mtu kama huyo?
Tungetamani kuwa bora, lakini hiyo ni ndoto ya mchana isiyoagulika. Katika hali ambapo kiongozi anawakandamiza watu, huwa anapata wawezeshaji wa kutosha kumdumisha mamlakani.
Wanaokandamizwa ni wanyonge mno kiasi cha kutowakabili nduli na wawezeshaji. Vinginevyo, basi wingi wa watu wema ungemtimua nduli huyo na wasaidizi wake wachache.
Hatungekuwa na vikongwe ving’ang’anizi kama Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda wala Paul Biya wa Cameroon.
Afrika ingekuwa bora kuliko Amerika, Wakenya hatungekaa kimya wabunge wetu wakikojolea na kuiyeyusha Sura ya Sita ya Katiba iliyomzuia mtu yeyote asiye mwadilifu hata kujaribisha ndoto ya kushikilia wadhifa wowote wa umma.
Kimsingi, uwepo wa viongozi wahalifu huakisi uovu na upumbavu wa wapigakura au watawaliwa, na haijalishi mazuzu hao wako wapi.
Ananiambia rafiki yangu mtema kimombo safi kwamba waovu, sawa na wapumbavu, wametapakaa kote duniani kwa usawa.
Jambo la busara ni kujichungua wenyewe kabla ya kukashifu nchi za watu na tawala zao, ili tuhakiki na kuhukumu kwa haki.
Mara nyingine utakapopata fursa ya kumchagua kiongozi – awe rais, gavana, seneta, mbunge au mwakilishi wa wadi – kumbuka yeyote utakayempa kura yako anawakilisha tabia na matamanio yako.
Haya basi, ngoja tuone una hulka gani.